Swaum Katambo, Katavi.
Awamu ya pili ya timu ya Madaktari bingwa 17 kutoka jijini New York nchini Marekani wamewasili hui leo Mei 4, 2024 mkoani Katavi kwa ajili ya kambi maalum ya kutoa huduma ya upasuaji wa kibingwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika.
Akizungumza mara baada ya kuwapokea madaktari hao waliowasili katika uwanja wa ndege wa Mpanda, Mganga Mkuu wa Wilaya ya hiyo Dkt. Alex Mrema amesema walitegemea kupokea madaktari bingwa 20 lakini watatu wamepata changamoto.
Amesema, timu hiyo inayotarajiwa kuwepo kwa siku saba itajikita katika sehemu kuu nne ambazo ni magonjwa ya kichwa na shingo (Head and neck surgery), Goita, upasuaji wote uliopo eneo la tumbo pamoja na upasuaji eneo la mataya pamoja na kurudisha sura.
“Tutatoa huduma ya upasuaji kwa sababu ‘tumeshascreen’ mpaka sasa hivi tuna wagonjwa 140 kwa hiyo tunategemea kadri tutakavyoweza kufanya kwa wingi tuwafikie walau wagonjwa 100,” amesema Dkt. Mrema.
Aidha ameongeza kuwa, Madaktari wa awamu ya kwanza waliweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa 69 ambapo kati yao wagonjwa 63 walifanyiwa upasuaji mkubwa.
Kwa upande wake Prof. Medhat Allam mmoja wa madaktari hao ambaye ni Mkurugenzi wa shirika la Operation International kwa niaba ya wenzake amesema wamefurahi kuja Tanzania, hivyo wanatarajia kufanya upasuaji wa wagonjwa wengi kwa kadri ya uwezo wao.
Nao baadhi ya Wananchi wa Mkoa wa Katavi, wamesema ujio wa madaktari hao utawaondolea changamoto ya upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa kuwa wagonjwa wanalazimika kupata rufaa kwenda Mbeya, Bugando, Benjamin Mkapa na Muhimbili kufuata huduma hizo kwa gharama kubwa.
“Wengine wanafariki kwa kushindwa kumudu gharama wanapopewa rufaa,hivyo tunashukuru ujio wao kwani ndugu zetu wagonjwa watapona bila kusafiri,” alisema Hamida Jumbe.
Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wa Shirika la Norbert & Friends Mission/ Operations International wameleta wataalam hao na hudum zitaendelea bila malipo hadi Mei 10, 2024.