Meneja Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amekiri kufurahishwa na kosa alilolifanya Mlinda Lango Abel Hussein na kuizawadia Geita Gold FC bao kwenye mchezo wa Ligi Kuu.

Simba SC ilikuwa mwenyeji wa Geita katika mchezo huo uliopigwa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam jana Jumanne (Mei 21), huku Mlinda Lango huyo aliyesajiliwa Msimbazi msimu huu akifanya makosa yaliyowapa nafasi wageni kutangulia kufunga bao dakika ya 10.

Ahmed Ally amesema kosa alilolifanya Abel Hussein halipaswi kuwa sehemu ya kumlaumu, zaidi ya kutambua kuwa linamkomaza ili aweze kuwa Mlinda Lango Bora kwa siku za usoni.

“Nimefurahi Abel Hussein kufanya lile kosa kwa sababu linamkomaza, yaani katika maisha yako yapende zaidi makosa yako kuliko mazuri kwa sababu makosa yako yanakufanya kuwa bora. Kosa alilolifanya uhakika ni kwamba hatolifanya tena katika michezo inayokuja, maana yake anazidi kuimarika.

“Namna ambavyo aliufuata ule mpira maana yake siku nyingine mpira kama ule ukija atakumbuka nilifanya kosa ataongeza umakini, aidha ataupangua ama atakaza mikono kuukamata. Kwa hiyo alivyofanya lile kosa nilisema ‘YES’ hasa ni muda wa Abel Hussein kupatia.

“Kwa hiyo sio kosa la kumlaumu ni kosa la kumkomaza, na watu wote bora duniani wamepitia makosa makubwa ndio maana wamekuwa bora, kwa hiyo kwa Abel Hussein kile ambacho amekifanya kinamuongezea thamani sasa. Na huyu ni Kipa ambaye tunamtegemea mno kwa msimu ujao, kwa hiyo ni lazima apitie matanuri ya moto ili aweze kukomaa. amesema Ahmed Ally

Katika mchezo huo Simba SC ilichomoza na ushindi wa mabao 4-1 yakifungwa na Saido Ntibazonkiza na Ladack Chasambi kila mmoja akifunga mabao mawili.

Man Utd, Bayern kuchangamkia fursa
Mkwanja wa Mwarabu kumsomba Ederson