Saa chache baada ya Klabu ya Chelsea kutangaza kuachana na Mauricio Pochettino, Klabu za Manchester United na Bayern Munich zimeanza kuhusishwa na mpango wa kumuajiri Kocha huyo kutoka nchini Argentina.

Chelsea imetangaza kusitisha Mkataba wa miaka miwili wa Kocha huyo, baada ya kufanya mazungumzo kwa kina na pande zote mbili kukubaliana kuvunjwa kwa Mkataba huo, ambapo hatua hiyo inamfanya Mauricio Pochettino kuwa huru kwa sasa.

Gazeti la The Standard limeibuka na taarifa zinazozitaja klabu za Manchester United na Bayern Munich kuwa miongoni mwa klabu ambazo huenda zikapigana vikumbo kuiwania saini ya Mauricio Pochettino.

Kwa sasa Manchester United wapo kwenye shinikizo la kumwacha Kocha Erik ten Hag, huku asilimi ndogo ya viongozi wakipendekeza Kocha huyo aachwe klabuni hapo kwa msimu mwingine.

Upande wa Bayern Munich wapo kwenye mpango wa kumsaka mbadala wa Kocha Thomas Tuchel ambaye anajiandaa kuondoka klabuni hapo baada ya kumaliza msimu wa 2023/24.

Kocha Mauricio Pochettino aliwahi kuhusishwa na klabu ya Manchester United miaka miwili iliyopita, kabla ya kuajiriwa kwa Erik ten Hag, hivyo huenda Uongozi wa Mashetani Wekundu wakatumia fursa kwa kumshawishi kuchukuwa nafasi ya kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi Klabu hapo.

Guardiola afunguka mafanikio 2023/24
Ahmed Ally: Nilifurahi Abel alipofanya makosa