Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imeombwa kukamilisha mchakato wa marekebisho ya sheria za habari zilizotolewa maoni na wadau ili kutoa mazingira rafiki kwa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao bila vikwazo.

Ombi hilo, limetolewa hii leo Mwei 23, 2024 na Wadau wa Vyombo vya Habari ambao wamesema kwa muda mrefu licha ya kutoa na kuwasilisha mapendekezo yao kuhusu mapungufu yaliyopo kwenye baadhi ya sheria hizo, bado utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua jambo linalopelekea mazingira magumu ya utendaji kazi.

Akiongea katika Maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa alieleza kuwa mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari umekuwepo kwa miaka mingi lakini bado sheria hizo ambazo nyingi ni za muda mrefu zimekwama kurekebishwa.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa.

Amesema, “sisi wengine tangu tuko Waandishi chipukizi tunazungumzia kupata hizi sheria mpya za habari, tangu 2008 kwa kweli ni muda mrefu, tunahitaji kusimamia jambo hili kwa umoja wetu na hatimae tupate sheria mpya za habari Zanzibar,” alieleza Dkt. Mzuri katika kongamano hilo.

Aliongeza wadau wa habari wamefanya mapitio ya sheria nane za habari ikiwemo Sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no.8 ya 1997, Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 iliyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010 na kuwasilisha ripoti ya mapendekezo yao kwa mamlaka husika ikiwemo kukutana na Rais na waziri.

Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania – MCT, Ernest Sungura amesema Vyombo vya Habari vitatekeleza kwa ufanisi wajibu wao katika kulinda mazingira iwapo waandishi watakuwa huru kupata na kutoa taarifa bila hofu kisheria.

 

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania – MCT, Ernest Sungura.

Ameongeza kuwa, “kaulimbiu ya kimataifa mwaka huu ilijikita katika uhifadhi wa mazingira. Lakini kwakweli bila kuwa na sheria nzuri za habari hatuwezi kutekeleza hayo tunayoyataka. Waandishi wa habari tunahitaji uhuru wa kupata taarifa ili tuweze kutekeleza uandishi wa habari mahususi. Hatuwezi kuyatekeleza hayo kama sheria hazitutengenezei mazingira ya kulinda uhuru wetu.”

Aidha, alivitaka vyombo vya habari kubuni mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kufikiria namna ya kuendana na kasi ya mageuzi ya masuala ya kiteknolojia ili kulinda uhuru wao akisema, “changamoto kubwa inayoathiri uhuru wa habari ni masuala ya kiuchumi. Tunaitaji kuangalia upenyo ili kuona namna gani kile kinachosababisha madhara katika vyombo vya habari kinatatuliwa.”

Akifafanua kuhusu maendeleo ya mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari Zanzibar, Katibu Mtendaji Tume ya Utangazaji, Suleiman Salim alisema, “kwa sasa mswada wa sheria ya habari ipo kwa Mwanasheria Mkuu, na tunaitegemea itakwenda baraza la wawakilishi kama mswada na tunawaomba walioko kule waichangie vizuri ili iweze kupita na tupate sheria mpya.”

Akichangia mdahalo kwenye maadhimisho hayo, Mwandishi wa Habari Mkongwe, Salim Said alieleza kuwa uwepo wa sheria bora ni muhimu katika kuwezesha mazingira bora ya waandishi wa habari kuwajibika akidai Vyombo vya Habari ni washirika wa maendeleo, hivyo kuwa na sera na sheria bora itawawezesha kuwa na mazingira rafiki katika kutekeleza majukumu yao.

Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari 2024, yameandaliwa Baraza la habari Tanzania Ofisi ya Zanzibar (MCT ZNZ), Chama cha Waandshi wa Habari Tanzania Zanzibar (TAMWA,ZNZ) Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA), Klabu ya Waandishi wa Wabari Zanzibar (ZPC) na Shirika la Commonwealth Foundation yakiambatana na kaulimbiu ya “UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NA MAGEUZI YA SERA NA SHERIA ZA HABARI ZANZIBAR.”

OSHA yatoa somo la usalama, afya kazini kwa Wabunge
Waandishi wawili jela kwa kutoa maoni ya uchochezi