Wakati Msemaji wa Brigedi za Al-Qassam, Abu Ubaida wa Hamas akitangaza kuwakamata wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza, Msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari amekanusha madai hayo akisema hakuna tukio la namna hiyo.

Kanusho Hagar amelitoa kupitia  mtandao wa X, huku Jeshi la Israel likiendelea kushambulia kwa mabomu Ukanda wa Gaza na maeneo ya mji wa Rafah, muda mchache baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuitaka Israel kusitisha mashambulizi na kuruhusu misaada ya kibinadamu.

Awali, katika hotuba yake Brigedia Al-Qassam alisema walifanikiwa kuwakamata wanajeshi hao kaskazini mwa Ukanda wa Gaza kwenye handaki na kudai kuwa hali zao ni majeruhi na wengine walifariki.

Kwa upande wao Madaktari wa Kipalestina walisema, zaidi ya watu 40 waliuawa katika mashambulizi hayo kwenye maeneo tofauti ya Ukanda huo.

WAKATI HAYO YAKIJIRI, huko Israeli maelfu ya watu wameandamana katika miji mbalimbali, wakitaka kurejeshwa kwa mateka wa Israel walioko Gaza, huku familia za waliotekwa zikimtaka Waziri Mkuu wa Taifa hilo, Benjamin Netanyahu kujiuzulu.

Maandamano hayo, yamefanyika ikiwa ni siku chache baada ya kutolewa kwa picha mjongeo inayoonyesha kutekwa nyara kwa watu ambao walichukuliwa mateka, huku Polisi wa Israel wakiwakamata baadhi ya waandamanaji.

Zelensky: Putin anatakiwa kujitafakari
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Mei 26, 2024