Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuleta mageuzi ya kilimo nchini kwa kukifanya kilimo biashara chenye tija kwa kuimarisha mnyororo wa thamani kutoka shambani hadi kwa mlaji.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo hii leo Agosti 3, 2024 alipofungua maonesho ya saba ya kilimo ya Nane Nane Zanzibar katika viwanja vya Dole , Kizimbani Mkoa wa Mjini.
Amesema Serikali itaanzisha vituo maalum kila wilaya kuhamasisha upatikanaji wa huduma kwa wakulima na wafugaji nchini.
Dkt. Mwinyi amesema Serikali inatarajia kutekeleza mradi mkubwa wa mageuzi wa uzalishaji wa wafugaji wa maziwa kwa wafugaji wadogo wadogo ambao utazingatia mabadiliko ya tabia nchi yenye gharama za shilingi bilioni 7.5.
Aidha, ametoa wito kwa vijana kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo na mifugo kwa kujiajiri , pia amewahimiza wajifunze mbinu bora za kilimo na ufugaji kupitia maonesho ya kilimo.