Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ametaja mikakati yake na chama chake baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa marudio walioususia ambapo ameahidi kuvuka mipaka kumchongea Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein na serikali ya CCM.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Maalim Seif alidai kuwa hawaitambui serikali hiyo kwakuwa haikupata ridhaa halali ya wananchi huku akiita ‘Serikali haramu’ na kuahidi kuibana mbavu ili ishindwe.

Maalim Seif alisema kuwa Chama chake kimepanga kuandaa taarifa maalum za kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana na kutangazwa marejeo ya uchaguzi uliofanyika Machi 20 mwaka huu, uliompa ushindi wa kishindo Dk. Shein na wawakilishi kupitia CCM na kwamba wataipeleka taarifa hiyo kwa jumuiya za kimataifa na mashirika ya kimataifa pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ili haki ipatikane.

Katika hatua nyingine, Maalim Seif aliziomba Jumuiya za Kimataifa na Wahisani kuchunguza akaunti za fedha za viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na za Dk. Shein, alizodai zimefunguliwa nje ya nchi.

Kadhalika, alizitaka jumuiya hizo kuwazuia viongoziwa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusafiri nje ya nchi.

“Natoa wito kwao kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya watawala hawa waovu ikiwa ni pamoja na kuwawekea vikwazo vya kusafiri, kufuatilia akanuti zao za fedha za nje ya nchi na kuchunguza matendo ya kihalifu dhidi ya binadamu. CCM lazima iwajibishwe kwa matendo yao maovu,” alisema Maalim Seif.

Mkataba Wa Neymar Wanaswa, Malipo Yake Yaanikwa Hadharani
WAKURUGENZI WAWEKWA KITANZINI