Mkataba wa mshambuliaji kutoka nchini Brazil na klabu ya Barcelona Neymar da Silva Santos Júnior, umevuja na kuanikwa hadharani, hatua ambayo imewashangaza walio wengi ambao waliamini alikua katika kiwango cha juu katika malipo ya mshahara wa kila juma.

Sehemu ya mkataba wa mshambuliaji huyo ambaye amekua chachu ya kusaka ushindi tangu alipojiunga na FC Barcelona mwaka 2013, imeonyesha analipwa kiasi cha Pauni elfu sabini na saba (77,000) kwa juma.

Mtandao wa Football Leaks, umethibitisha kupata nakala ya mkataba wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 wenye kurasa 13, na kujiridhisha ni halali, kutokana na uwepo wa saini ya Neymar.

Sehemu hiyo ya malipo yake ya kila juma, inaonyesha Neymar analipwa kiasi cha Pauni million 5, kwa mwaka na ukokotozi ulipofanyika imebainika kiasi anachokichukua kila mwishoni mwa juma ni Pauni elfu sabini na saba.

Hatua hiyo imechukuliwa kama njia rahisi kwa klabu ambazo zinahitaji kumsajili mwishoni mwa msimu huu ikiwepo Man Utd, kupata ahuweni wa kumng’oa Camp Nou tofauti na ilivyokua siku za nyuma, ambapo iliaminika huenda mshahara wake ukawa kikwazo.

Kurasa nyingine za mkataba wa Neymar zimefafanua namna anavyolipwa ongezeko la fedha ya ziada (Bonus), endapo atafikia mafanikio yanayohitajika kwenye klabu ya Barcelona ambayo kwa sasa ndio bingwa wa barani Ulaya.

Ifuatayo ni sehemu ya vipengele ambavyo vinampa nafasi mshambuliaji huyo kupokea ongezeko hilo la fedha za ziada (Bonus)

  1. Endapo Neymar atacheza kwa asilimia 60 ya michezo yote ndani ya dakika 45 akiwa na Barcelona analipwa Euro 1,062,500.
  2. FC Barcelona inapofanikiwa kufuzu kucheza michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, mshambuliaji huyo kutoka Brazil anapokea kiasi cha Euro 637,500.
  3. FC Barcelona inapofanikiwa kufuzu kucheza hatua ya mtoano kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, Neymar anapokea kiasi cha Euro 425,000.
  4. Neymar analipwa kwa mafungu tofauti endapo FC Barcelona itachukua ubingwa wa michuano tofauti, ubingwa wa La Liga anapewa Euro 637,500; ligi ya mabingwa barani Ulaya Euro 850,000 na kombe la Mfalame (Copa del Rey) analipwa Euro 850.000.

Kama Barca itatwaa ubingwa wa barani Ulaya (Champions League) pamoja na kombe la Mfalme (Copa del Rey), Neymar analipwa Euro 1,062,500 na ikitokea Barcelona wanatwaa ubingwa wa vikombe vitatu kama ilivyokua msimu uliopita, mshambuliaji huyo anachukua Euro million 1.7.

Malipo haya yanafanyika endapo Neymar atacheza asilimia 50 na kuendelea ya michezo ya michuano yote kwa msimu mzima katika michuano hiyo mitatu.

Endapo itatokea Neymar anatangzwa kuwa mchezaji bora wa dunia na kutwaa tuzo ya Ballon d’Or, FC Barcelona wanamlipa Euro 425,000.

Mama Kanumba alia Lulu kumtupa, aomba 'japo salaam'
Maalim Seif amchongea Dk Shein na CCM