Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amesema Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limefuta matokeo ya mitihani ya nadharia (theory) kwa masomo yote ya Programu ya Utabibu Ngazi ya Tano (NTA Level 5).
Dkt. Sichalwe amesema hayo leo, wakati akitoa taarifa kuhusu “kuvuja mitihani ya utabibu” mbele ya Waandishi wa habari waliofika kusikiliza taarifa hiyo katika ukumbi wa Wizara ya Afya Jijini Dodoma.
“Katika kikao cha 78 cha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi kilichokaa tarehe 01 Novemba, 2021 taarifa hiyo ilijadiliwa, kupitia Sheria ya Baraza Sura 129 na Kanuni za Mitihani, Kifungu 33 (1) (iii), 2004 (GN.75) limefuta matokeo ya mitihani ya nadharia (theory) kwa masomo yote ya Programu ya Utabibu Ngazi ya Tano (NTA Level 5).” Amesema Sichalwe
Ameendelea kusema kuwa, Baraza limeagiza kurudiwa kwa mitihani hiyo upya ndani ya wiki sita kuanzia tarehe 1 Novemba, 2021, huku akisisitiza mitihani hiyo ifanyike sambamba na mitihani ya marudio (Supplementary Examinations) kwa programu zingine za afya nchi nzima.
Aidha, Dkt. Sichalwe amewaelekeza Wakuu wa vyuo vyote vya afya kuwapa taarifa wanafunzi ili wajiandae kwa ajili ya mitihani hiyo inayotarajiwa kurudiwa.
Hata hivyo Dkt. Sichalwe amesema, Wizara imesikitishwa na tukio hilo na itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kukamilisha uchunguzi na kuwachukulia hatua wale wote walioshiriki kufanya udanganyifu huo.