Polisi nchini Afrika Kusini wanachunguza tukio la kupatikana kwa takriban miili 21 inayoshukiwa kuwa ni ya wachimbaji haramu iliyopatikana karibu na mgodi unaotumika katika mji wa Krugersdorp, katika eneo la Krugersdorpma lililopo magharibi mwa jiji la Johannesburg.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, imeeleza kuwa miili 19 kati ya hiyo iligunduliwa siku ya Jumatano alasiri na mingine miwili imegunduliwa asubuhi ya alhamisi huku ikisema wanashuku kuwa miili hiyo, ilihamishwa toka eneo jingine hadi mahali ilipopatikana, ambayo ni mgodi wa kibinafsi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi katika eneo hilo, Brenda Muridili amesema, “Tunaweza kuthibitisha kwamba asubuhi ya leo timu yetu ya utafutaji na uokoaji ilirejea kwenye eneo la tukio na, walipokuwa wakitafuta, waligundua miili miwili zaidi. Walizipata kutoka shimoni (mgodini) wazi.”
Mapema mwezi Julai 2022, wanawake wanane wa kikundi cha filamu walibakwa na kuuliwa katika mgodi uliotelekezwa katika eneo hilo, ambapo walikuwa wakifanya kazi ya upigaji picha za video za muziki kisa ambacho kilizusha maandamano ya ghasia dhidi ya wachimba migodi haramu katika jamii zinazowazunguka.
Wiki iliyopita, mashtaka ya ubakaji na wizi dhidi ya wanaume 14, ambao pia wanashukiwa kuwa wachimba migodi haramu, yaliondolewa baada ya polisi kushindwa kuwahusisha na ubakaji huo kupitia ushahidi wa DNA.
Uchimbaji haramu wa madini umeenea nchini Afrika Kusini, huku wachimba madini wanaojulikana kama “zama zamas” wakitafuta dhahabu katika migodi mingi ambayo haijatumika na iliyotelekezwa ndani na karibu na mkoa wa Johannesburg.