Vilio na simazi vimetawala wakati mwili wa Robson Mazengo (25), ambaye ni kati ya Dereva bodaboda wawili na abiria mmoja waliofariki katika ajali baada ya gari la mali ya ofisi ya mkuu wa mkoa Morogoro lenye namba za usajili T.514 CAQ toyota Land Cruisser kugonga gari la jeshi la Wananchi (JWTZ) lenye namba za usajili 2032JW 12 aina ya Ashok Leyland kisha kupoteza muelekeo kuwagonga watu hao waliokua kwenye Pikipiki.
Dar24 Media, imefika nyumbani ulipo msiba Mtaa wa Mgulu was Ndege kata ya Mkundi na kuzungumza na Baba wa Marehemu, Mazengo Kisena ambaye amesema mtoto wake amefariki ameacha mke na mtoto mmoja na kuiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia mtoto na mke wa Marehemu kwani alikua tegemezi katika familia hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa Morogoro, Fortunatus Musilimu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la alfajiri ya Desemba 5, 2022 eneo la Magunila kata ya Kihonda Manispaa ya Morogoro, Barabara Kuu ya Morogoro kuelekea Dodoma.
Aliwataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Robson Mazengo (25) dereva bodaboda ,Faustine Kolineli (28), Dereva Bodaboda na Ashirafu Yussuph (43) abiria alikua kwenye bodaboda wote wakazi wa Manispaa ya Morogoro.
Chanzo cha ajali hiyo, kinatajwa kuwa ni uzembe wa dereva wa gari lenye usajili T.514 CAQ mali ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, ambalo lilikua linaendeshwa na Dereva Abeid Namangaye kwa kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, na kwa sasa anashikiliwa na jeshi la Polisi.