Rais wa marekani, Joe Biden ameidhinisha kupelekwa kwa msaada wa dharura katika jimbo la New York kufuatia dhoruba kali ya theluji iliosababisha vifo vya zaidi ya 27 huku wengine maelfu wakiachwa bila nishati ya umeme.
Kikosi cha dharura cha uokoaji, kimejitahidi kuokoa wakaazi walioathiriwa kutokana na dhoruba ya theluji ya karne ambayo imesababisha vifo vya zaidi ya watu 50 nchini humo na kutatiza mwenendo mzima wa usafiri hasa katika majimbo tisa.
Gavana wa New York, Katheleen Hochul amesema wanatazamia dhoruba itarejea tena ambapo barafu yenye urefu wa nchi 6 hadi 12 upande wa kusini wa Kaunti ya Erie na kusini kidogo mwa eneo hilo walipata theliji yenye urefu wa nchi 30 hadi 40 na hivyo ni mapema kutabiri kama ndio mwisho.
Amesema, “Ofisi ya idara ya afya Erie imethibitisha vifo 25 katika kaunti yote ya Erie, idadi hiyo inajumuishwa na ile ya mji wa Buffalo na wapo baadhi ambao wanaweza kupatikana ambao idara ya afya haijawathibitisha.”
Mamlaka katika jimbo la New York imeeleza hali kuwa mbaya zaidi hasa katika eneo la Buffalo huku miili ikigunduliwa kwenye magari, kingo za theluji na waokoaji wamekuwa wakikagua gari kwa gari wakitafuta waliofariki au walio hai.
Kikosi cha ulinzi cha taifa, pamoja na timu zingine za uokoaji wameokoa mamia ya watu kutoka katika gari zilizofunikwa na theluji na nyumba ambazo hazina umeme, lakini mamalaka imesema kwamba watu zaidi huenda wamenasa kwenye theluji.