Wafanyakazi watatu wa kituo cha Televisheni ya kibinafsi ya Baba Tv nchini Uganda, wamefukuzwa kazi baada ya kukejeli kura iliyopigwa bungeni, katika matangazo yaliyokuwa yakirushwa hewani moja kwa moja.
Kupitia taarifa ya kituo hicho, imeeleza kuwa kilipokea malalamiko dhidi ya mtangazaji Simon Muyanga Lutaaya, ambaye Jumanne (Januari 24, 2023), alitania kuhusu onyo lililopigiwa kura na wabunge dhidi ya Waziri wa Makazi, Persis Namuganza.
Kituo cha Baba TV, chenye makao yake makuu jijini Kampala, kimesema baadhi ya wabunge pamoja na maafisa kutoka Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC), shirika linalodhibiti vyombo vya Habari, wamelalamikia matamshi hayo.
“Walalamikaji waliona picha hizo kama za kufedhehesha, kudhihaki na kukejeli taasisi ya bunge, viongozi wake na waheshimiwa wabunge na sisi tunawajibika kwa kuchukua hatua za ndani kuzuia hili kutokea katika siku zijazo, ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kwa timu nzima ya wanahabari hao,” ilieleza taarifa ya Baba TV na kuomba radhi kwa Bunge na UCC.