Serikali nchini, imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo mashirika yasiyo ya Kiserikali katika masuala ya Afya kutokana na michango yao kwa jamii.
Hayo yamebainishwa Jijini Arusha kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Dkt. Tumaini Haonga wakati akifunga kikao kazi cha Wadau wa Maendeleo na Serikali cha kuainisha vipaumbele na mikakati ya utekelezaji mwaka 2023/2024.
Amesema, “tumekuwa tukishirikiana na Wadau wa Maendeleo kuhudhuria kikao hiki muhimu, sisi kama Serikali tunashukuru sana kwa ujio wenu mmeacha majukumu yenu lakini tumekusanyika kwa pamoja na kikao hiki kitakuwa na matokeo chanya kwa ajili ya kuweka mipango yetu kwa maslahi mapana ya taifa.”
Aidha, ameongeza kuwa wadau wa Maendeleo wana umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa Afua za Elimu ya Afya hivyo Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha Ustawi wa Afya Bora unaendelea kuimarika kwa Watanzania.