Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, kuhakikisha wanamfikisha katika vyombo vya sheria baba anayetuhumiwa kumlawiti mtoto wake mwanafunzi wa darasa la pili (7).

Majaliwa ametoa agizo hilo, wakati akisalimia watoto katika kituo cha kulelea Watoto yatima cha Mandaliwa kilichopo Mbweni Jijini Dar es saalam, baada ya hivi karibuni kusambaa kwa taarifa ikimuonesha mtoto huyo anayedaiwa kulawitiwa na baba yake mzazi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Amesema, Serikali inakemea vikali vitendo vya unyanyasaji, ubakaji na ulawiti kwa watoto, hivyo imewataka Wakuu wa mikoa na makamanda wa Polisi nchini kuhakikisha wanawasaka na kuwachukulia hatua kali za kisheria, watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo viovu.

Aidha, Majaliwa amesema katika siku za hivi karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya wazazi, walezi na wanajamii kuwafanyia watoto vitendo vya ukatili ikiwemo ulawiti, hivyo kuwasababishia maumivu na msongo wa mawazo hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kuendelea na masomo.

Serikali kuendeleza ushirikiano na wadau masuala ya afya
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Februari 18, 2023