Wafanyakazi wa kike wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited – GGML ladies, wametoa msaada wa vifaa tiba mbalimbali kwa akina mama Wajawazito na Wazazi katika hospitali ya Nzela na kituo cha Afya Kasota zilizopo Halmashauri ya Wilaya Geita.
Akizungumza mara baada ya kutoa msaada huo, Makamu mwenyekiti wa kikundi hicho, Lina Sitta amesema wanawake wanaofanya kazi GGML wameguswa na changamoto za uhaba wa vifaa tiba katika vituo vya afya katika vijiji vinavyowazunguka.
Amesema, “Tumeona tuanze na vijiji vya Kasota na Nzela vilivyopo karibu na mgodi wa GGML tumeona akina mama wakikosa sabuni, taulo za mama waliojifungua na nepi za watoto. Msaada huu ni maalum kwa ajili ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani.”
Naye Mganga Msaidizi wa kituo cha afya Kasota, Stanley Victor amewashukuru Wanawake hao kwa kutoa msaada na GGML kusaidia ujenzi wa maabara, nyumba ya mtumishi na jengo la baba na mtoto kituoni hapo.
Amesema, “Mmeitendea haki siku ya wanawake duniani mwaka huu.Wagonjwa wengi waliopo hapa wamefarijika sana kutokana na msaada huu,” huku kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani mwaka huu ikiwa ni Ubunifu na mabadiliko ya teknolojia: chachu katika kuleta usawa wa kijinsia.