Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amethibitisha kuhusu maisha yake ya hapo awali huku akieleza namna ambavyo alikuwa ni mtumiaji mzuri wa Pombe ambayo aliiacha baadaye baada ya kuokoka na sasa ameamua kuwapigania Vijana waiache.
Akizungumza katika mkutano na wadau ili kumaliza pombe na matumizi ya dawa za kulevya katika Kaunti ya Nakuru, Gachagua amesema anawaomba wale wote waliojikita katika matumizi ya kinywaji hicho kuhakikisha wanaacha mara moja ili kuepuka madhara ya ulevi.
Amesema, “Rais, Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki na wengine wengi hawajawahi kuwa na shida na pombe. mimi nakiri kuwa nilikuwa nakunywa pombe sana kabla sijaokoka na wakati nilipoacha, mambo yangu yamekuwa yakinyooka.”
Hata hivyo, ameongeza kuwa operesheni ya kuwasaka wauza pombe imekuwa na changamoto kutokana na baadhi ya maafisa wa polisi kujihusisha na uuzaji wa kinywaji hicho, na kudai kuwa ili mambo yabadilike ni lazima kila mmoja kuwajibika.