Mwanasheria Mkuu wa wilaya ya Kaunti ya Los Angeles George Gascón ametangaza kuwa Daniel Saldana, ambaye sasa ana umri wa miaka 55, ameachiliwa huru baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 45 jela mnamo mwaka 1990 kwa kosa la kufyatulia risasi gari iliyokuwa ikitoka kwenye mchezo wa soka wa skuli moja ya sekondari iliyoko kwenye bustani ya Baldwin, mashariki mwa Los Angeles.

Ufyatuaji risasi huo ulipelekea kujeruhiwa vijana wawili kati ya sita waliokuwamo ndani ya gari hilo lakini hawakufariki.

Saldana alikuwa mmoja wa wanaume watatu walioshtakiwa kuhusika na shambulio hilo na akahukumiwa kifungo jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa sita ya kujaribu kuua na shtaka moja la kufyatulia risasi gari lililokuwa na watu ndani yake.

Hata hivyo ushahidi uliotolewa na mshambuliaji mwingine wa tukio hilo aliyehukumiwa ulibainisha baadaye kwamba Saldana “hakuhusika kwa namna yoyote ile katika ufyatuaji risasi na wala hakuwepo wakati wa tukio hilo.”

Mwanasheria Mkuu wa wilaya ya Kaunti ya Los Angeles amemuomba msamaha Saldana na familia yake, akisema, “ninajua kwamba hii haitakurudisha nyuma ya miongo uliyosota gerezani, lakini natumai kuomba kwetu radhi kutakupa faraja japo kidogo wakati unaanza maisha yako mapya”.

Gascón ameongezea kwa kusema: “sio tu hili ni janga la kuwalazimisha watu kufungwa gerezani kwa uhalifu ambao hawakufanya, lakini kila pale haki inapokosa kutendeka kwa ukubwa kama huu, wahusika halisi huwa wangali wako nje wakifanya uhalifu mwingine”.

Kufikia Februari 2020, jumla ya watu 2,551 waliofutiwa mashtaka baada ya kuhukumiwa na kufungwa jela walitajwa katika Masijala ya Taifa ya Waliosamehewa nchini Marekani. Muda wote ambao watu hao walioachiliwa huru walisota magerezani unafika miaka 22,540.

Mmomonyoko wa maadili: Taasisi ya kidini yasitishiwa usajili
Wasimamizi miradi watakiwa kukamilisha kazi kwa wakati