Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa ametaka kuanzishwa kwa Kurugenzi maalum itakayoshughulikia masuala ya kupambana na ujangili wa wanyamapori ili kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori, huku akimteua Kamshina Msaidizi wa Uhifadhi, John Antony Nyamhanga kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Kudhibiti Ujangili nchini.
Mchengerwa ametoa kauli hiyo kwenye hafla ya uzinduzi wa mkakati wa kitaifa wa kudhibiti ujangili 2023- 2033 na mkakati wa usimamizi wa Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyama za Jamii jijini Dodoma, huku akiwaomba watanzania kuacha tabia ya ujangili na kusisitiza kuwa kwa sasa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kufanya ujangili.
Amesema, taasisi za uhifadhi za Wizara yake (NCAA, TANAPA, TAWA na TFS) chini ya mfumo wa Jeshi la uhifadhi zinatakiwa kushirikiana katika kutekeleza mikakati hiyo na kukamilisha mara moja Mkakati wa Kitaifa wa Rasilimali Fedha kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mikakati hiyo.
Aidha, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye idadi kubwa ya wanyamapori na imetenga zaidi ya theluthi ya ardhi yake kwa ajili ya uhifadhi wa Wanyamapori hivyo ni muhimu kuwa na kurugenzi kamili ambayo itasaidia kulinda na kuhifadhi wanyamapori.
Amefafanua kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya simba, chui, nyati na ni ya tatu kwa idadi ya tembo duniani ambapo amesema hiyo inatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi wa wanyamapori.
Aidha, amesema utalii unachangia zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni na asilimia 17 ya pato la Taifa ambapo amesisitiza kuwa uhifadhi wa rasilimali hizi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla na amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuutangaza utalii kupitia Royal Tour.