Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Gianni Infantino amesema atalipa kipaumbele bara la Afrika katika mipango ya maendeleo ya soka, katika kipindi chote cha uongozi wake.
Infantino amezungumza hayo wakati wa ziara yake nchini Uganda, ambayo ilitanguliwa na zile za Afrika kusini na Zimbabwe juma lililopita.
“Nimedhamiria kulipa kipaumbele bara la Afrika, na dhamira hii nilikua nayo tangu nilipotembelea kwa mara ya kwanza mwaka uliopita. Nimeanza kwa kuonesha jambo hili kwa vitendo kwa kumteua mwanamke wa Afrika kuwa katibu mkuu wa FIFA, Fatma Samoura,” Alisema Infantino akiwa jijini Kampala.
“Afrika ina vipaji vya soka ambavyo vinahitaji kuendelezwa kwa kuwekea miundo mbinu kama ilivyo kwenye mataifa mengine barani Ulaya na kwingineko,” aliongeza.
Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la Uingereza (BBC), Infantino alikutana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ikulu, na kisha alifanya mkutano na viongozi wa FUFA siku ya Jumamosi.
Pia shirika hilo limeripoti, kiongozi huyo wa soka duniani, alishuhudia mchezo wa vijana chini ya umri wa miaka 17 kati ya KCCA FC dhidi ya Lweza FC, kabla ya kuelekea Rubaga kufungua kituo cha michezo.
Mbali na hayo, Infantino aliahidi kuanza kuyafanyia kazi masuala yote ya maendeleo ya soka la Afrika kwa kuishirikisha kamati ya utendaji ya FIFA kuanzia mwaka huu na kuendelea.
“Afrika itaanza kuona faida za maendeleo ya soka kutoka FIFA, na ninatarajia kuona bingwa wa dunia akitoka kwenye bara hili” aliongeza kiongozi huyo.