Mabingwa wa soka Tanzania bara Young Africans hawana matumaini ya kuwatumia washambuliaji wao tegemezi, Amissi Tambwe na Donald Ngoma kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Aprili 1, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Meneja wa Young Africans, Hafidh Saleh amesema Mrundi Tambwe na Mzimbabwe Ngoma wote wanasumbuliwa na majeraha, na huenda wakaanza mazoezi mepesi juma lijalo.
Hafidh amesema uwezekano wa wawili hao kuwa tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Azam Aprili 1 ni mdogo, kwa sababu bado wanasumbuliwa na maumivu.
“Wote wanaendelea na matibabu, wakati tunakwenda Zambia walipewa wiki mbili za mapumziko, maana yake wana moja zaidi ya kuendelea kuwa nje. Hivyo kuwatarajia kuwa tayari kucheza wiki ijayo ni vigumu,”amesema Hafidh.
Wawili hao wote wamekuwa wakisumbuliwa na maumivu, Tambwe goti na Ngoma kifundo cha mguu baada ya kuumia kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, visiwani Zanzibar.
Pamoja na hayo, kutokana na umuhimu wao katika klabu na pia kukosekana kwa washambuliaji wengine walio tayari, wachezaji wote hao wamewahi kutumika kwa kulazimishwa kabla ya maamuzi ya kupumzishwa wiki iliyopita.