Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoani Tanga kimepata pigo baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Muheza, Rwebangira Mathias Karuwasha kutangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokana na chama hicho kupoteza dira na mwelekeo.
Hatua ya mwenyekiti huyo kutangaza kujiuzulu imekuja siku chache baada ya maamuzi ya Mkutano Mkuu wa viongozi wa chama kanda ya kaskazini Mkoani Tanga uliokuwa chini ya Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe kuridhia kuvunja uongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya ya Mkoa wa Tanga.
Aidha, akitangaza uamuzi huo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari Jijini Tanga, Rwebangira Karuwasha amesema hayo ndio mambo makubwa yaliyopelekea kuamua kukaa pembeni na kujiunga na CCM ambako anaona kuna sera makini zinazotekelezeka.
“Kwa mfumo wa uongozi unaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe haukubaliki na hakuweza kuvumilia, sitegemei kuendele kuwepo kwenye chama hicho kilichokuwa cha watwana na watumwa hivyo nimeridhia kujiunga na CCM, “Amesema Rwebangira.
Hata hivyo amesema kuwa chama pekee ambacho kina dira na sera zinazoeleweka ni CCM, hivyo muda wowote kuanzia sasa atajiunga nacho.