Rapa Eminem ameamua kuchukua hatua kwa vitendo kufuatia shambulizi la kigaidi lililochukua uhai wa watu 22 katika tamasha la muziki la Ariana Grande jijini Manchester nchini Uingereza, kwa kuchangisha fedha kuwafuta machozi familia zilizowapoteza wapendwa wao.
Rapa huyo ametumia mtandao wake wa Twitter wenye wafuasi zaidi ya milioni 20 kuwahamasisha watu kuchangia fedha ili kufanikisha lengo lake.
“Tafadhali niunge mkono katika kuwasaidia waathirika wa Manchester na familia zao, kwa kuchangia kupitia @BritishRedCross na @MENnewsdesk,” alitweet.
Eminem pia aliwaelekeza wafuasi wake kwenye ukurasa wa ‘JustGiving’ ambao alijiunga nao hivi karibuni kwa lengo la kuchangia waathirika, alipotoa tangazo kuwa atarudi jijini Manchester kufanya tamasha lenye faida kwa waathirika. Hadi sasa ukurasa huo umeshachangisha zaidi ya $2.2 million.
Katika hatua nyingine, Eminem amewaonjesha mashabiki wake mpango wa kuwapa kitu kipya kwenye tamasha lake la kumbukumbu ya miaka 15 ya albam yake ya tatu ‘The Eminem Show’.