Naibu Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Mduduzi Manana amejiuzulu nafasi hiyo kufuatia kashfa ya kumshambulia mwanamke katika klabu moja ya usiku.
Manana ambaye alipandishwa kizimbani wiki iliyopita kujibu tuhuma zilizomkabili amekuwa akijitetea kuwa alijikuta akifanya kitendo hicho alichokiri kuwa ni cha aibu baada ya kuchokozwa na kughafirika.
Taarifa kutoka Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imeeleza kuwa barua ya Manana ya kujiuzulu imepokelewa na kukubaliwa. Ofisi hiyo ilimshukuru kwa muda wake aliotumia kuwatumikia wananchi na mchango alioutoa kwa Serikali.
Aidha, Chama chake cha African National Congress (ANC) kimesema kimepokea kwa heshima taarifa za kujiuzulu kwa Manana na kumshukuru kwa muda wake alioutumia kukitumikia chama hicho.
- Serikali yakiri kuwepo mgogoro wa Bombadier, wanasiasa watajwa kuuchochea
- Ummy Mwalimu aagiza kuboreshwa kwa huduma za afya
Awali, ANC walilaani vikali kitendo hicho na kueleza kuwa vitendo vya kuwashambulia wanawake havikubaliki na kwamba ni vitendo vya aibu.
Manana aliomba radhi kwa kitendo alichokifanya akieleza kujutia uamuzi aliouchukua aliodai kuwa ulitokana na kughafirishwa.