“Sikuvaa hirizi, mwamuzi alinikagua na kudhibitisha sikuwa na kitu kinachoashiria ushirikina. Hata kamisaa wa mechi alijiridhisha.”

Mshambuliaji wa Simba raia wa Senegal, Pape Abdoulaye N’daw ameomba asamehewe kwa tukio lilitokea kwenye mechi dhidi ya Prisons.

Akizungumza na Soka360, Pape aamesema hakuvaa hirizi kama inavyodaiwa na kuzungumzwa lakini anaomba asamehewe kwani tamaduni za uvaaji zinatofautiana kwenye nchi mbalimbali.

“Sikuvaa hirizi, mwamuzi alinikagua na kuthibitisha sikuwa na kitu kinachoashiria ushirikina. Hata kamisaa wa mechi alijiridhisha.”

Huku akionekana kuwa na huzuni na majonzi kuhusiana na tukio lenyewe, Pape amesema walinzi wa Prisons walikuwa wanapata taabu kumkaba kutokana na tofauti ya kimo kati yao.

“Mara nyingi mabeki wa Prisons walikuwa wanaishia kunisukuma kutokana na ufupi wao, mmoja wao alinishika na kugusa fulana nyeusi ya ndani niliyokuwa nimevaa pamoja na mkanda wa asili unaopendwa kuvaliwa na watu wa Senegal na Gambia kama sehemu ya utamaduni wa uvaaji wetu”

“Watu wa Afrika Magharibi tuna uvaaji wetu, ni sehemu ya utamaduni wetu lakini naomba nisamehewe kama nimekosea. Sitarudia kuvaa hivyo kwenye mechi japo napata ugumu kuelewa kwa nini watu wametafsiri kuwa ni uchawi. Sijui wamepata wapi uzoefu wa kutofautisha uvaaji unaoshiria ushirikina na ule usioashiria?”

Pape amesema yeye ni muislam safi asiyeamini kwenye ushirikina. “Mimi ni muislam, siamini ushirikina. Kamwe ushirikina si ngazi ya kupata mafanikio kwenye maisha.”

“Silaha yangu kuu ni kujituma. Ukiwauliza wachezaji wa Simba au makocha wangu, watakwambia daima mimi huwa wa kwanza kufika mazoezini na kufuata masharti yote ya timu kila mahali tunapokwenda”

Licha ya kuomba asamehewe, Pape amedai kushangazwa na jinsi vyombo vya Habari vilivyoripoti tukio hilo bila kumpa nafasi ya kumsikiliza.

“Niliambiwa kulikuwa na waandishi wengi kwenye mechi hio lakini hakuna hata mmoja aliyenifuata kunihoji. Walikimbilia kuripoti walichosikia na bado wanaendelea kuandika bila kunifuata kunihoji. Angali picha wanazoweka kwenye magazeti, wanaonesha fulana nyeusi ya ndani niliyovaa siku hio na kudai ni hirizi.”

“Mimi sio mwandishi, ila nafikiri mtu yeyote makini hufanya kazi kwa kusikiliza pande zote. Mtu makini na mpenda ukweli angeweza kuujua undani wa tukio kwa kumuuliza kamisaa, mwamuzi aliyenikagua na mimi mwenyewe muathirika kabla ya kuandika vitu vinavyouchoma moyo wangu mpaka sasa.”

Msenegali huyo amemalizia kwa kusema, “Inauma kuhukumiwa kwa kosa ambalo sikulitenda, lakini inauma zaidi kuhukumiwa bila kupewa haki ya kusikilizwa, ni sawa na kunyimwa haki mara mbili. Hata mtuhumiwa ana haki. Hata hivyo naomba nisamehewe.”

Kesi Ya Mita 200 Kukatiwa Rufaa
Magufuli Ajisogeza Zaidi Kwa Wafanyakazi