Baada ya Bunge kusema wametuma fedha za matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu tangu Septemba 20, Hospitali ya Nairobi imekiri kupokea fedha kutoka Tanzania zikiwa hazina maelezo na wanafanya kuzifuatilia.

Hayo yamesemwa na Afisa wa Kitengo cha Habari na Itikadi wa Chadema, Hemed Ali ambapo amesema kuwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya imethibitisha kupokea fedha kutoka Tanzania lakini zikiwa hazina maelezo.

Jana Ofisi ya Bunge ilitoa taarifa kuelezea mchakato wa utumaji wa fedha hizo kiasi cha Sh 43 milioni zilizochangwa na Wabunge wa Tanzania ikisema kuwa pesa hizo zilitumwa tangu Septemba 20.

Aidha, Ofisi ya Bunge ililazimika kutoa ufafanuzi kuhusu fedha hizo ikiwa ni muda mfupi tu baada ya taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari,ambapo alisema kuwa michango mingi alikwishapokea isipokuwa mchango huo wa wabunge uliokuwa na thamani ya milioni 43.

“Wamenieleza kuna fedha zimeingizwa kutoka Tanzania ila hazina maelezo ndiyo wanafuatilia benki,” amesema Ali

Hata hivyo, Ali ambaye yupo Jijini Nairobi amesema kuwa amethibitishiwa na Hospitali ya Nairobi kuwa wamepokea fedha hizo kutoka Tanzania ingawa kulikuwa hakuna maelezo zaidi.

Magazeti ya Tanzania leo Septemba 24, 2017
Vijana nchini watakiwa kuchangamkia fursa