Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema agizo la Rais huwa halipingwi na mtu yeyote na akawataka watumishi wa umma kote nchini wazingatie suala hilo.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo mwishoni mwa wiki (Machi 25, 2023) wakati akizungumza na Watumishi, Wakuu wa Idara na Wakuu wa Taasisi za Mkoa wa Simiyu, kkatika kikao kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Amesema, “agizo la Rais likishatolewa halipingwi na mtu yeyote, kinachofuata ni utekelezaji na siyo kukaa vikao na kupitisha maamuzi mengine ya kulipinga. Hili ni suala la itifaki, na ni la muhimu sana Serikalini.”
Kauli ya Waziri Mkuu, ilikuja baada ya kumhoji Mkurugenzi Mtendaji wa Busega ni kwa nini hajatekeleza agizo la Rais la kujenga soko katika eneo la Lamadi, na badala yake wakaamua kulipeleka eneo la Nyashimo.
“Busega ni kwa nini hamtekelezi maagizo ya Mheshimiwa Rais ya kujenga soko eneo la Lamadi lakini mmeamua kulipelekea Nyashimo? Iweje madiwani mnakaa tena vikao na kuanza kujadili maelekezo ya Mheshimiwa Rais?” alihoji Waziri Mkuu.
Akijibu swali hilo, Mkurugenzi huyo Veronica Sayore alisema wameshampata Mhandisi Mshauri ambaye ni Wakala wa Majengo nchini (TBA), ambapo Waziri Mkuu naye akaielekeza TBA wafanye hiyo kazi Lamadi na siyo Nyashimo.