Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amewataka wananchi kuwa na amani na kuondoa mazingira ya taharuki kufuatia ajali ya ndege iliyotokea ziwani mjini Bukoba, kwani hali ni shwari na zoezi la uokoaji linaendelea vyema.
Chalamila ameyasema hayo mapema hivi punde leo Novemba 6, 2022 wakati akihojiwa na Dar24 eneo la ajali na kuongeza ndege hiyo ilishindwa kutua uwanja wa ndeege wa Bukoba kutokana na matairi kupata hitilafu na kushindwa kutoka hivyo Rubani kuamua kuitua mtoni ili kuepuka madhara zaidi.
Miili mitatu isiyotambuliwa yakutwa Baharini
Amesema, “Niwasihi wananchi muondoe taharuki maana hali ni shwari na msije mkasababisha madhara zaidi kwa kuwa na hofu, ndege imetua hapo kutokana na hitilafu lakini mawasiliano na marubani yanaendelea vizuri na tunaangalia uwezekani ili tuivute kuitoa mtoni.”
Chalamila ameongeza kuwa, tayari wamefanya mawasiliano na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye kamati ya maafa ipo chini yake, ikiwemo kupokea maelekezo kwa Rais Samia kuwa waendelee na zoezi vizuri bila kutokea kwa hitilafu zaidi.
Aidha, amefafanua kwamba atakuwa akitoa taarifa kila baada ya masaa mawili ili kuona kama kuna jipya lililojitokeza na kwamba kwasasa zoezi la uokozi bado linaendelea hivyo watu wapunguze taharuki kwani Serikali ipo kwa ajili ya kuhakikisha usalama wao na mali.
Mapema asubuhi ya leo, zilienea taarifa za ajali ya Ndege hiyo mali ya Kampuni ya Precision Air, ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, William Mwampaghale alisema juhudi za uokoaji katika ajali ya Ndege iliyotokea Ziwa Victoria zinaendelea kufanywa na Jeshi la Zimamoto na Jeshi la Wananchi (WTZ), kwa kushirikiana na Wavuvi.