Mwanamke mwenye umri wa miaka 20 nchini India amejifungua mara mbili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, ambapo amefanikiwa kupata mapacha siku 26 baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza.
Arifa Sultan alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume mwishoni mwa Februari mwaka huu, kwa mujibu wa Daktari wake, Sheila Poddar ambaye ni mtaalam wa afya ya uzazi. Alisema baada ya kujifungua kawaida mama na mtoto wake waliruhusiwa na hospitali ya Ad-Din iliyoko Dhaka.
Daktari huyo ameeleza kuwa baada ya wiki nne, Sultan alifikishwa tena kwenye hospitali hiyo na akiwa analalamika kuwa na maumivu tumboni. Baada ya madaktari kumfanyia vipimo (ultrasound), walibaini kuwa alikuwa na mapacha tumboni.
“Wakati wa uzazi wa kwanza, hakufanyiwa ultrasound kwa kuwa alikuwa katika hali nzuri, hivyo hali ya kuwa na watoto watatu tumboni haikubainika,” ameeleza Dkt. Poddar.
Ameeleza kuwa tukio hilo sio la kawaida na ni vigumu kutokea, lakini huweza kuwatokea baadhi ya wanawake kutokana na hali ya afya yao ya uzazi.
“Tunashukuru watoto wote watatu wana afya nzuri na wako salama na. Mapacha walitolewa tumboni kwa mama kwa njia ya upasuaji,” alisema.
Kwa mujibu wa Shirika la Taifa la Afya nchini humo, tukio hilo ni adimu kutokea kwa akina mama na kwamba wastani wake wa kutoekea ni 1 kati ya milioni, na kwamba kutobainika kabla ya kujifungua kuna uwezekano mdogo zaidi.
Mkuu wa kitengo cha afya ya uzazi katika hospitali ya Max Healthcare, Dkt. S.N Basu ameeleza kuwa hali hiyo ni rahisi kuwatokea wanawake walioko vijijini kwani wengi hawapati nafasi ya kufanyiwa vipimo.
“Huko vijijini, watu wengi hawafahamu kuhusu afya zao za uzazi kabla. Hawajui ni watoto wangapi ambao wako tumboni wakati wa ujauzito na wakati mwingine hata hawajui kama ni wajawazito kwa kipindi husika,” Dkt. Basu anakaririwa na Dailymail.