Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu amesema yapo malalamiko kuwa baadhi ya Walimu wanaojitolea wanawasilisha barua feki zinazosema wanafanya hivyo wakati hawajitolei.
Ametoa kauli hiyo leo Mei 25, 2021 Bungeni Dodoma wakati akimjibu Mbunge wa Longido Dk Stephen Kiluswa aliyehoji ni kwanini Serikali isiajiri Walimu ambao wanajitolea.
Waziri Ummy, amesema kuna kazi kubwa kukamilisha mchakato wa ajira zaidi ya 6000 kwa sababu wamebaini kuna udanganyifu katika baadhi ya maeneo.
Ajira za walimu zilizotangazwa ni 6,949 lakini Ummy amesema hadi juzi watu 89,958 walikuwa wameomba nafasi hizo idadi ambayo ni kubwa na wapo watakaokosa nafasi hizo.
“Tunajitahidi kufanya hivyo lakini bado kuna kazi hata huko, tunapokea barua nyingi za waliojitolea lakini nyingi zimebainika kuwa ni feki kwa hiyo tuna kazi na tunaomba Spika mtuamini tutatenda haki,” amesema Ummy.