Wakati watu katika maeneo tofauti duniani wakijifikiria mara kadhaa kabla ya kuamua kupata chanjo ya Corona hata kwa hatua ya kwanza, katika hali isiyokuwa ya kawaida babu mmoja kutoka nchini India mwenye umri wa miaka 84, amekamatwa baada ya kudai kuwa amedungwa chanjo 11 ya virusi vya Corona.

Brahmadeo Mandal mwenye umri wa miaka 84, mkazi wa jimbo la Bihar Mashariki alifanikiwa kupokea dozi hizo kwa kutumia vitambulisho tofauti na nambari za simu za jamaa zake.

Wanasema za mwizi ni arobaini na basi za mzee huyo zilifika alipokuwa amekwenda kwenye kituo cha afya akiwa anataka kupata dozi ya 12 akielezea nia yake Mandal alisema serikali imefanya jambo la maana na ndio sababu yake ya kupata chanjo kupita kiasi.

Mandal alisema kuwa alipokea chanjo yake ya kwanza Februari 13, mwaka 2021, na baadaye alikuwa akipokea chanjo kila baada ya mwezi kuanzia Machi, Mei, Juni, Julai na Agosti na kisha alichomwa chanjo tatu mwezi Septemba akitumia kitambulisho tofauti tofauti kikiwemo cha mpiga kura.

Kulingana na mzee huyo, kufikia mwishoni mwa mwaka 2021, alikuwa tayari ameshapokea jumla ya chanjo 11 na kuongeza kuwa anahisi vizuri.

Inawezekana Mzee Mandal aliamua kupokea chanjo kwa wingi kutokana na tafiti zinazosema wanaume waliopona Corona hushindwa kutungisha mimba, ambapo utafiti uliofanywa nchini Ubelgiji umebaini kuwa mbegu za kiume za wanaume walioambukizwa virusi vya corona huwa dhaifu kwa muda wa wiki tatu baada ya kupona.

Kulingana na utafiti huo, wakati wa kipindi hicho waathiriwa hushindwa kutungisha mwanamke mimba. Matokeo ya utafiti huo yaliyochapishwa kwenye jarida la Fertility and Sterility, yalibaini kuwa mbegu za kiume za waathiriwa hukosa uwezo wa kusafiri katika mfumo wa uzazi wa mwanamke hivyo, hushindwa kufikia yai la mwanamke.

Akamatwa na jino la Tembo darini
Watu watano wajeruhiwa ajali ya basi Tabora.