Mwanaume mmoja mwenye silaha amefyatua hovyo risasi na kuwaua askari wawilio wa kike wa jeshi la polisi na raia mmoja Mashariki mwa jiji la Liege nchini Ubelgiji.
Katika tukio hilo lililofanyika leo, mtu huyo pia ameripotiwa kumteka mfanyakazi wa usafi na kumtumia kama kinga, kabla ya kuuawa na askari wa jeshi la polisi waliofika katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la nchini humo la RTBF, mshambuliaji huyo aliachiwa hivi karibuni kutoka jela kuwa chini ya kipindi cha matazamio alipokuwa akitumikia kifungo cha makosa ya dawa za kulevya.
Ingawa bado haijafahamika chanzo cha uamuzi wa mshambuliaji huyo kufanya tukio la mauaji, Serikali ya Ubelgiji imesema kuwa inalichukulia tukio hilo kama tukio la kigaidi na kwamba huenda mtu huyo alifundishwa ugaidi alipokuwa amefungwa jela.
Meya wa Liege, Willy Demeyer amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la mauaji alipofanya mkutano na waandishi wa habari. Meya huyo amesema kuwa watatoa msaada wa kisaikolojia na vitendo kwa familia za marehemu.
Muendesha mashtaka wa Serikali amesema kuwa tukio hilo limetokea leo majira ya asubuhi karibu na mgahawa katikati ya jiji hilo. Amesema kuwa mshambuliaji aliwanyemelea askari, akamchoma kisu askari mmoja na kumnyang’anya bunduni kabla ya kuanza kufyatua risasi.