Mzee Abdallah Chasamba (96) ambaye anasema alikuwa ni kati ya watu wa kwanza kuanzisha Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa – JKT, Ruvu baada ya uhuru mwaka 1961 amesema hatosaua siku ambayo aliitwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere mara tatu na kushindwa kuitika kutokana na taratibu za Kijeshi.
Mzee Chasamba ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano maalum na Dar24 Media nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa kitendo hicho kilimpa ushujaa kwani Makamanda wa Kikosi cha Jeshi walimsifia kwa Rais Nyerere kwa kusema anastahili pongezi kwa si rahisi kufanya hivyo kwa kiongozi wa nchi.
“Ilikuwa ni siku ya passin out paredi, Mwl. Nyerere anapita na mimi nilikuwa mstari wa kwanza mbele na ukiwa ditesheni hutakiwi kuangalia upande wowote zaidi ya macho mita 100 mbele, akaja pale kaniona kaniita ‘Abdallah…Abdallah…. ndio umemaliza ukamanda umekuwa mwanajeshi kweli,’ mie sikumjibu,” anasimulia Mzee Chasamba.
Amesema, “akaniita mara kwanza sijaitika, mara ya pili sijaitika mara ya tatu mie pia sikuitika ikabidi apite huku anacheka mbele kidogo akamuuliza yule Kamanda akasema yule katokea Ikulu na tunafahamiana sana tangu tunadai Uhuru yule lakini hata anashindwa kuniitika, ndipo yule Kamanda akamjibu wale Askari ni 400 na katika wote wale yule (Mzee Abdallah) ndiye Kamanda.”
Mzee Abdallah anasema Kamanda yule aliendelea kumwambia Mwl. Nyerere kuwa hata yeye hakutarajia iwapo asingeitika lakini amefanya hivyo kutokana na taratibu za Jeshi za kutotaka kujibu chochote, kugeuka kushoto au kulia na kuinama au kuangalia juu, ukiwa kwenye ditesheni.