Mahakama ya Ujerumani imemuhukumu kifungo cha miaka 14 gerezani, mwanaume mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kuua na kudhuru mwili katika shambulizi la kutumia kisu kwenye treni mwaka 2021.
Katika shambulizi hilo, watu wanne walijeruhiwa na Mwanaume huyo raia wa Palestina mwenye umri wa miaka 28 ambaye amekulia nchini Syria, akitambuliwa kama Abdalrahman ambaye amekutwa na hatia katika mahakama ya Munich.
Waendesha mashtaka, ambao walidai shambulizi hilo lilikuwa lenye msimamo mkali wa kiislamu waliitaka Mahakama itoe hukumu ya kifungo cha maisha jela huku mawakili wa mshtakiwa wakisema mteja wao alikuwa mgonjwa na hangeweza kushtakiwa kwa uhalifu na walitaka aachiwe huru.
Shambulizi hilo, lilifanyika katika treni za mwendo kasi, ICE iliyokuwa ikisafiri kutoka Passau kwenda Hamburg Novemba 6, mwaka 2021.