Vyombo vya usalama jijini Conakry nchini Guinea vinamshikilia mwanamke mmoja kwa kosa la kuwapa ujauzito ‘feki’ wanawake jijini humo na kujipatia fedha nyingi kutoka kwao kinyume cha sheria.

Zaidi ya wanawake 200 waliofika katika kituo cha polisi anakoshikiliwa mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina la N’Fanta Camara walieleza kuwa mwanamke huyo ambaye ni mganga wa kienyeji aliwapa dawa aliyodai itawafanya wapata ujauzito ndani ya kipindi kifupi.

Wanawake hao wamedai kuwa baada ya kuanza kutumia miti shamba waliyopewa na Camara, walianza kujisikia kuwa na dalili za ujauzito ikiwa ni pamoja tumbo lao kuongezeka ukubwa, kichefuchefu, kutapika na homa.

Hata hivyo, wanawake hao walioendelea kupata tiba kutoka kwa Camara katika kila hatua ya ‘ujauzito’ huo wanadai tofauti na ujauzito wa kawaida, waliendelea kupata siku zao (hedhi) huku wengine wakivuja damu nyingi wakati huo.

Wameeeza kuwa mwanamke huyo aliwakataza kwenda hospitalini kupima kwani hata wakipima madaktari hawatauona ujauzito.

Wanawake hao waliamua kwenda polisi baada ya baadhi yao kukaa na matumbo makubwa kwa miezi 12 hadi 16 bila kujifungua huku wakiwa na dalili zote za ujauzito.

“Siku ambayo alikuwa anatupima kwa mkono na kutueleza kuwa ‘una ujauzito’ tulikuwa tunampa vitenge na kuku, hiyo ni baada ya kumpa franc 300,000 (Sawa na $564, Sawa na 1,2040,000 TZS),” alisema mwanamke mmoja aliyepewa mimba feki.

Akijibu tuhuma hizo mbele ya waandishi wa habari katika eneo la Sousou akiwa chini ya polisi, mtuhumiwa huyo alieleza kuwa yeye alikuwa anawapa dawa lakini aliwaambia wazi kuwa anayeweza kutoa ujauzito ni Mungu pekee.

“Mwanamke alipokuja kwangu, kitu cha kwanza nilimuuliza kama anamuamini Mungu. Baada ya hapo niliwaambia kuwa ni Mungu pekee anayetoa mtoto na sio mimi. Ninafanya kazi kubwa kusaidia wanawake kufanikisha ndoto zao za kuwa mama lakini mengine namuachia Mungu,” alisema Camara.

Bi. Camara akizungumza na vyombo vya habari

Mkuu wa kitengo cha uhalifu, Moussa Tiergboro amesema kuwa mwanamke huyo alikuwa anaingiza fedha nyingi kwa siku kwa udanganyifu.

“Yaani kama alikuwa anatembelewa na wanawake 50 kila siku, ina maana alikuwa anaingiza 450 francs ($846, sawa na 1,861,200 TZS).

Ummy Mwalimu aridhishwa na kasi Muhimbili
Serikali yatoa shilingi bilioni 24.4