Askofu mmoja wa Kanisa la Kianglikana Kenya (ACK) alifikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya kujaribu kumbusu na kumshika mwanamke akitumia nguvu bila idhini yake.
Askofu huyo Joel Waweru, wa Kanisa la Kianglikana Kenya (ACK), alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kibra, Derrick Kuto siku ya Jumanne, Januari 11, 2022 na anakabiliwa na mashtaka wa unyanyasaji wa kingono.
Katika stakabadhi za mashtaka zilizowasilishwa mahakamani hapo, mtumishi huyo wa Mungu anatuhumiwa kufanya kitendo hicho tarehe tofauti mtaani Lang’ata, katika kaunti ya Nairobi.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, mwanamke huyo alilalamika kuwa Waweru amekuwa akimwambia mara kadhaa kuwa anavutiwa na urembo wake na alikuwa akimsifia na kumtaka kimapenzi licha ya kufahamu alikuwa ni mke wa mtu.
Mahakama iliarifiwa kwamba mwanamke huyo hata alishushwa cheo katika kanisa alilokuwa, baadaye akahamishiwa akapelekwa katika kanisa tofauti na mshahara wake ukakatwa.
Ripoti ya polisi ilisema mwanamke huyo alilalamika kwamba askofu huyo kwa nyakati tofauti alimwaibisha, na kumtaka awaambie waumini kwamba hajawahi kumwagiza washiriki ngono kama uvumi ulivyodai.
Ripoti ya polisi inaeleza zaidi kuwa siku moja akiwa na doa kwenye blauzi yake, mtumishi wa Mungu alifika ofisini mwake na kumshika matiti mahali doa lilikuwa kwa njia isiyofaa, jambo ambalo lilimfanya akose raha na utulivu.
Inasemekana kwamba askofu huyo alimuita mbele ya wazee wa kanisa na kudanganya kuwa aliwaita “ihii”, kumaanisha wanaume ambao hawajatahiriwa na alimsababishia aibu na kuchanganyikiwa kihisia na kuhisi kutokuwa salama
Taarifa zinaendelea kusema kuwa hulka ya askofu huyo ilimkera sana mwanamke huyo na kumfanya kutoa ripoti polisi kuhusu suala hili baada ya kuchoshwa.
Waweru pia alikabiliwa na mashtaka ya pili ya kumshika mwanamke huyo matiti bila idhini yake mnamo Julai 13, 2021 na ripoti ya polisi inasema kuwa, mshtakiwa anasemekana kumnyanyasa mwanamke huyo kingono tangu 2018.
Hata hivyo, Waweru alikanusha mashtaka hayo na kuomba apewe dhamana isiyokuwa na masharti makali ambapo ombi lake lilikubaliwa na kuachiliwa kwa dhamana ya KSh50,000.