Mwanaharakati aliyekuwa mstari wa mbele kupinga utawala uliosheheni ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, Askofu Mkuu Mstaafu Desmond Tutu amezikwa leo 01.01.2022.

Maombolezo makubwa kwa ajili yake yalifanyika kwenye kanisa kuu la jiji la Cape Town, St George`s Cathedral ambapo amezikwa.

Maombolezo yalianza kwa “Zaburi” na msafara wa makasisi waliochoma ubani na kuwasha mishumaa ndani ya Kanisa ambamo kwa miaka na miaka Askofu Mkuu Tutu alitumia mimbari kupambana na utawala wa kibaguzi wa makaburu.

Mazishi yake yamekuwa ya aina yake kuwahi kufanyika ambapo maiti yake iliyeyushwa kwa kemikali na jivu lake kuhifadhiwa katika kanisa la St. Georges Cathedral.

Watu nchini Afrika Kusini wamekuwa wanaomboleza kwa muda wa wiki nzima baada ya kifo cha askofu huyo aliekuwa na umri wa miaka  90.

Askofu mkuu wa Cantebury Justin Welby ambae ni kiongozi wa Kanisa Anglikana duniani amesema, “Tutu alileta mwangaza pale ambapo tulikuwamo katika kiza. Akiongeza kuwa Askofu mkuu Welby amesema kumsifu Askofu mkuu Tutu ni sawa na panya kumvisha tembo koja shingoni.”

Askofu huyo Mkuu wa Cantebury amesema Afrika Kusini imetoa mfano wa viongozi mahiri, Nelson Mandela na Desmond Tutu waliotunukiwa nishani ya Amani ya Nobel. Welby ameeleza kuwa tofauti na wengine waliotunukiwa nishani hio, nyota ya Desmond Tutu  imeendelea kung’ara.

Tutu hakutaka mazishi ya kifahari hivyo watoto na wajukuu zake waliyatekeleza maombi yake.

Jeneza lake lilikuwa la kawaida na maelfu ya watu miongoni mwao wale waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali za nchi walitoa heshima zao mwisho.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema watu wa Afrika kusini wanamshukuru Askofu Mkuu Desmond  Tutu kwa yote aliyofanya kwa manufaa ya nchi yao.

Pia amemshukuru Tutu kwa mchango mkubwa aliotoa katika harakati za kuung’oa utawala wa makaburu.

Rais Ramaphosa amesema askofu Mkuu Tutu alikuwa mpiganaji wa mstari wa mbele katika harakati za kuleta uhuru, usawa na amani siyo tu nchini Afrika Kusini bali duniani kote na ilitokana na uadilifu wake.

Kifo cha Askofu mkuu Tutu ni pigo kubwa kwa watu wa Afrika wanaomwita Askofu huyo Baba. Tutu alizaliwa mnamo mwaka 1931 magharibi mwa jiji la Johannesburg na kwanza alifanya kazi ya uwalimu na alitawazwa kuwa kasisi mnamo mwaka 1961.

Bien wa Sauti Sol aibiwa
Makamu wa Rais ashiriki Misa ya Mwaka mpya