Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango akiwa na Mkewe Mama Mbonimpaye Mpango leo tarehe 1 Januari 2022 wameungana na waumini wa kanisa katoliki Parokia ya mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo Kuu la Dodoma kushiriki Misa Takatifu ya sherehe za Bikira Maria mama wa Mungu pamoja na kumshukuru Mungu kwa mwaka mpya 2022.

Akizungumza na waumini hao mara baada ya kumalizika kwa misa hiyo Makamu wa Rais Dkt. Mpango amewasihi waumini na watanzania wote kuendelea kumshukuru Mungu kwa kuvuka salama mwaka 2021 kwa kuwa mwaka huo ulikuwa na changamoto nyingi zikiwemo za maradhi ya Uviko19. Amewaomba waumini hao kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake ili waweze kuongozwa na hekima ya Mungu katika kuwatumikia watanzania.

Aidha Makamu wa Rais amesema ni muhimu kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kupanda mazao ya muda mfupi na muda mrefu kulingana na maeneo husika. Amewasihi wananchi wa Dodoma pia kutumia mvua hizo kupanda miti katika maeneo yao ili kulinda mazingira pamoja nakuupendezesha mkoa wa Dodoma uliokabiliwa na upungufu wa mvua kwa muda mrefu.

Amesema wazazi wanapaswa kuwaongoza watoto wao na kuwalea katika maadili mema ikiwemo kukabiliana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. Amewatakia watanzania wote kuwa na mwaka 2022 wenye Amani na kusisitiza kila mmoja akatimize wajibu wake kwa Mungu na kwa Tanzania.

Askofu Desmond Tutu apumzishwa kwenye nyumba yake ya milele
Watu 12 wafariki kwa mkanyagano kuukaribisha mwaka mpya