Kiungo na Nahodha wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile, kesho Alhamis (Julai 15) anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha maafande hao wa Jeshi la Magereza, kitakachocheza dhidi ya Biashara United Mara FC, Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Asukile ataonekana kwa mara ya kwanza akiwa na Tanzania Prisons, baada ya kutumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitano na faini ya Sh 500,000, liyotolewa na Shirikisho la soka nchini TFF, mwezi Mei.

Kamati ya mashindano ya TFF ilimuadhibu Asukile, kufuatia makosa ya kutoa maneno ya kejeli, kashfa, udhalilishaji na shutuma dhidi ya Young Africans, wachezaji wa kigeni wa klabu hiyo pamoja na mwamuzi wa mchezo na TFF, alioyatoa baada ya mchezo wa hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho.

Asukile alisema, “Sisi hatujakwama popote ila tumeshindwa kucheza kwa kuwa wenyewe walikuwa wametuzidi kwa kuwa wamemuongeza refa uwanjani, kwa hiyo kama umemuongeza refa uwanjani sisi hatuwezi kumshinda refa, ila kwa wachezaji sisi tuliwazidi”.

Mchezo kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Biashara United Mara, utaanza kuunguruma kesho Alhamis (Julai 15), saa 8:00 mchana.

Hayati Mkapa aliichukia Rushwa kwa vitendo
Azam FC: Yakubu bado mchezaji wetu