Mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri ameagiza kuwekwa ndani saa 48 mkuu wa kitengo cha manunuzi ugavi wa halmashauri ya Mji Njombe, Jackobo Kichibi baada ya kutoa taarifa ya uongo kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa.
Agizo la mkuu wa wilaya huyo limekuja mara baada afisa manunuzi huyo kutakiwa kuonyesha mkataba wa kuanza kwa mradi wa maduka ya biashara(Pombe Shop)iliyogarimu zaidi ya milioni 300 ambapo taarifa za awali zilikinzana na alizokua akimueleza kiongozi wa mbio za mwenge.
‘’Nimesikitishwa sana kuona kwamba mtumishi kama huyu anawadanganya viongozi wa mbio za mwenge wa kitaifa…siwezi kukuacha lazima nikuchukule hatua…nakuagiza OCD umchukue huyu akakae ndani saa 48’’ amesema Ruth.
Awali kiongozi wa mbio za Mwenge, Charles Kabeho alifika katika mradi wa maduka biashara(Pombe Shop)kwa ajili ya kuzindua lakini kabla ya jambo hilo kufanyika alitaka kuona mikataba ili kujua ni lini mradi huo unatakiwa kuanza kutokana na kukosa huduma ya vyoo.
‘’Naweza nikafungua ila naomba mniridhishe kwa kuona mikataba ili nijue mradi huu unapaswa kuanza lini…lakini pamoja na hayo nimezungukia mradi ambao nimeona hauna huduma ya vyoo..jambo ambalo linashangaza kutokana na ukubwa wa mradi huu alafu hakuna vyoo’’ amesema Kabeho.
‘’Nilimuuliza huyu afisa manunuzi huu mradi ulipaswa kuanza lini lakini alinambia ni julai 1 wakati nilivyosoma mkataba unasema ni juni 1…sipendi kudanganywa ninapokuuliza maswali yangu jibu kama inavyotakiwa’’ amesema Kabeo.
Hata hivyo kiongozi huyo wa mbio za Mwenge alikaataa kugawa Pikipiki kwa watendaji wa vijiji baada ya kuwa na Plate Namba za njano za biashara badala ya zile nyeupe na kuwa na alama ya Serikali pamoja na umiliki ukiwa ni wa mzabuni.
‘’Hizi Pikipiki ni za Serikali lakini jina la umiliki ni la mzabuni siwezi kuzigawa, maana huu ni ufujaji wa fedha za Serikali…, haiwezekani mnunue nyinyi alafu muweke plate namba za biashara.., sasa hizi zitafanya kazi ya wananchi au inaenda kufanyiwa biashara’’ amesema
Aliongeza kuwa kitengo cha manunuzi katika halmashauri hakina msaada na Serikali badala yake kimekuwa kikiipa hasara kutokana na kutokuwa wazalendo katika matumizi ya fedha.
‘’Ningekuwa na uwezo kitengo cha manunuzi katika halmashauri ningekifuta maana kimekuwa sio msaada bali kimekuwa kikiongeza gharama tu Serikalini…, bora ukanunue kwanza utalipa kwa kawaida na wakati’’ amesema Kabeho.
Katika halmashauri ya mji wa Njombe alikataa kuzindua pia vyumba viwili vya madarasa ambapo kwa upande wa na wilaya ya Njombe alikataa mradi wa jengo la mama na mtoto lililogharimu zaidi ya milioni 60 ambazo hazilingani mradi ulivyotekelezwa.