Umoja wa Afrika (AU) unafanya mazungumzo na Jamuhuri ya Madagascar, ili kupata data za kiufundi kuhusu usalama na ufanisi wa dawa ya mitishamba iliyotangazwa hivi karibuni kutibu Covi-19.
AU imesema kuwa Kamishna wa tume ya Umoja wa Afrika inayohusika na masuala ya kijamii Amira ElFadil alifanya mazungumzo na balozi wa Madagascar nchini Ethiopia Eric Randrianantoandro tarehe 30 April na wameafikiana kuwa nchi wanachama wataupatia maelezo muhimu Muungano wa Afrika kuhusu dawa za mitishamba.
Imeelezwa kuwa baada ya kupata maelezo Umoja huo kupitia kituo chake cha udhibiti wa magonjwa – (Africa CDC), kitatathimini data zilizokusanywa kuhusu usalama na ufanisi katika tiba hizo asili dhidi ya virusi vya corona.
Dawa hiyo inahusishwa na mmea wa Kichina unaoitwa Artemisia (pakanga) – ambao ni mojawapo ya miti ambayo huchanganywa pamoja na mimea mingine ya Madagascar kama tiba ya ugonjwa wa Malaria.
Hata hivyo AU imesema kuwa tathimini yake ya madawa ya mitishamba itazingatia maadili ya kiufundi ya kidunia katika kukusanya ushahidi muhimu wa kisayansi kuhusu ufanisi wa mitishamba.
Marais wa Tanzania, Jamuhuri ya Congo, Guinea Bissau na Equatorial Guinea wote wamemaua kutuma ndege nchini Madagascar kuchukua dawa hiyo ya mitishamba ili kuwapa wananchi wao.