MOTO unatarajia kuwaka kesho ndani ya Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, pale Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakapovaana na wenyeji wao Tanzania Prisons.

Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ambao ni wa kiporo, unatarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na historia ya timu hizo kila zinapokutana.

Mpaka sasa rekodi baina yao inaonyesha kuwa wamekutana mara 11 kwenye mechi mbalimbali za ligi, mechi tano wameenda sare huku kila timu ikishinda mara tatu.

Azam FC ambayo inauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo huo hasa ikitaka kurejea kileleni, bado imekuwa ikipata shida kubwa kila inapocheza na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, kwani haijafanikiwa kushinda mechi hata moja ikiwa imepoteza mara mbili na sare tatu ndani ya dimba hilo.

Jumla ya mabao 20 yamefungwa na timu hizo katika mechi zote 11 walizokutana, cha kustaajabisha zaidi kila timu imefunga mabao 10 jambo ambalo linaongeza zaidi mvuto kwenye mchezo wa kesho.

Wakati timu hizo zikitarajia kuchuana, Azam FC imeonekana kuwa na rekodi nzuri ya ufungaji mabao mpaka sasa ikiwa imefunga mabao 34 (wastani wa bao 1.9 kila mchezo) na kufungwa 11, walioing’arisha kwenye ufungaji ni Kipre Tchetche aliyefunga tisa, John Bocco nane na Shomari Kapombe akitupia saba.

Tanzania Prisons yenyewe ina wastani wa kufunga bao moja kwenye kila mchezo msimu huu baada ya kufunga mabao 19 ndani ya mechi 19 huku ikiruhusu kufungwa angalau bao moja kila mechi ikiwa imeruhusu mabao 18, staa wao mkubwa anayewapaisha ni mshambuliaji Jeremiah Juma aliyetumbukiza mpira nyavuni mara 11 mpaka sasa.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo wa kwanza dhidi ya Prisons uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, ikiichapa mabao 2-1 yaliyofungwa na Kipre Tchetche na Farid Mussa.

Vilevile ikumbukwe kuwa itaingia dimbani ikiwa na morali ya hali ya juu baada ya kutoka kushinda mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City Jumamosi iliyopita katika mchezo ambao Azam FC ilionyesha kiwango bora zaidi hasa kipindi cha pili.

Tanzania Prisons yenyewe imetoka kucheza ugenini na kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya maafande wenzao wa Mgambo JKT ya Tanga, mchezo uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema utakuwa mgumu kwani hivi sasa Tanzania Prisons ni timu bora sana Mbeya hivi sasa baada ya Mbeya City kupotea, huku akidai kuwa wamejipanga kushinda na kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi.

“Itakuwa ni ngumu, kwani si kazi rahisi siku zote kucheza na timu ya jeshi, Yanga walikuja hapa wakalazimisha sare baada ya kuokolewa na mwamuzi dakika za mwisho kwa kupewa penalti (2-2), Simba imepoteza hapa (1-0) dhidi yao, watataka kuendeleza hilo, lakini sisi tumejipanga vema kupat ushindi,” alisema.

Hall alisema jambo kubwa watakaloingia nalo ni kucheza kwa nguvu pamoja na kujaribu kumiliki mpira kwa muda wote wa mchezo ili kuwanyima nafasi Prisons.

“Tuna nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo na hii ni kama wachezaji watacheza vema kama walivyofanya katika mechi yetu ya mwisho dhidi ya Mbeya, hasa staili waliyocheza kipindi cha pili,” alisema.

Mwingereza huyo aliongeza kuwa amebaini ya kuwa wapinzani wake wanatumia nguvu sana ikiwemo kubebwa na maumbile ya wachezaji wake ambayo ni makubwa wakiwa ni warefu.

“Awali nilipanga kumchezesha Messi (Ramadhan Singano) katikati, lakini baada ya kuwaona wachezaji wa Prisons jana, nimeamua kumpa nafasi ya Michael Bolou atayesaidiana na Migi (Jean Mugiraneza) na Sure Boy (Salum Abubakar), ili kukabiliana na aina ya uchezaji wa Prisons, hivyo Messi ataanza kwa kucheza pembeni,” alisema.

Matajiri hao wa Azam Complex, watawakosa wachezaji wake watano kwenye mchezo huo, kiungo Himid Mao atakayekuwa akitumikia adhabu ya kukosa mchez mmoja baada ya kukusanya kadi tatu za njano.

Wengine watakaoikosa ni mabeki Aggrey Morris, Racine Diouf na Abdallah Kheri na mshambuliaji Didier Kavumbagu, ambao wote ni majeruhi na wako kwenye maandalizi ya mwisho kurejea uwanjani.

Ushindi wowote wa Azam FC kesho utaifanya kupanda kileleni kwenye msimamo wa ligi kwa kufikisha jumla ya pointi 48 na itaiacha Yanga itakayobakia na pointi 46 katika nafasi ya pili huku Simba inayoshika nafasi ya tatu ikiwa nazo 45.

Baada ya mchezo huo Azam FC itakuwa imebakiwa na mchezo wake mmoja wa kiporo sawa na Yanga, itakaocheza dhidi ya Stand United, utakaofanyika Machi 16 mwaka huu ndani ya Uwanja wa Azam Complex.

Juventus Vs Bayern Munich, Guardiola Asaka Namna Ya Kuondoka Kwa Heshima
African Lyon Wajipanga Kufanya Usajili Wa Haja