Klabu bingwa ya Afrika mashariki na kati Azam FC, leo saa 10.30 jioni itawakaribisha JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Azam FC iliyojikusanyia jumla ya pointi 59 katika nafasi ya pili, imepania kushinda mchezo huo ili kuendelea kuifukuza Yanga kwenye mbio za ubingwa na kama ikiukosa basi ijidhatiti katika nafasi yake hiyo inayowaniwa pia na Simba yenye pointi 58.

Lakini kwa mujibu wa msimamo ulivyo Yanga ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kama itajikusanyia pointi nne tu katika mechi zake tatu zilizobakia, yaani ushindi mchezo mmoja na sare tu.

JKT Ruvu yenyewe iliyojizoelea pointi 25 katika nafasi ya 14 ipo kwenye vita kali ya kupigania kushuka daraja ikiwa chini ya Kocha wake, Abdallah Kibadeni ‘King’, ambapo katika mechi zao sita zilizopita imejikusanyia pointi 10 tu ikishinda tatu vipigo viwili na sare moja.

Akizungumzia mchezo huo Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema ni lazima washinde ili waendelee kujiweka sawa kwenye msimamo wa ligi huku wakisikilizia matokeo ya Yanga inayoongoza.

Hall aliongeza kuwa kikosi chake cha leo kitakuwa na mabadiliko kidogo hasa baada ya kuwakosa baadhi ya nyota wake beki Aggrey Morris na kiungo mkabaji Jean Mugiraneza ‘Migi’, anayesumbuliwa na majeraha ya mguu aliyoyapata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba.

Morris anakosekana baada ya kukusanya kadi tatu za njano ya mwisho akiipata dhidi ya Simba ikiwa ni kadi yake ya kwanza katika ligi tokea arejee uwanjani, hivyo leo atatumikia adhabu ya kukosa mchezo huo mmoja.

Wachezaji wengine ambao Azam FC itaendelea kuwakosa ni mabeki Pascal Wawa, Shomari Kapombe na Wazir Salum, ambao ni bado ni wagonjwa na winga Farid Mussa aliyeko kwenye majaribio nchini Hispania.

Lakini habari njema zaidi ni kurejea kikosini kwa nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, aliyemaliza adhabu yake ya kutumikia kadi nyekundu aliyopata wakati Azam FC ikiipiga Mtibwa Sugar bao 1-0 ndani ya Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Vilevile mshambuliaji Allan Wanga naye atarejea kikosini baada ya kupona majeraha ya mgongo aliyopata wakati Azam FC inapambana na Mwadui kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Azam FC itaingia uwanjani  ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa timu hiyo mabao 4-2 katika mchezo wa kwanza uliofanyika ndani ya Uwanja wa Karume, Dar es Salaam mwaka jana.

Mabao ya Azam FC yalifungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga mawili, Didier Kavumbagu na Kipre Tchetche, huku yale ya JKT yakitupiwa na Najim Magulu na Samwel Kamuntu.

Kihistoria mpaka sasa tokea Azam FC ipande daraja mwaka 2008 na kuanza kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008/09, imekutana na JKT mara 15 na kushikilia rekodi ya kuishinda mara nyingi zaidi ikiwa imeichapa mara nane huku Wanajeshi hao wakiibuka kidedea mara nne na mechi tatu zikiisha kwa sare.

Jumla ya mabao 36 yamefungwa ndani ya mechi hizo, Azam FC ikishinda robo tatu ya mabao hayo yote ikiwa imeingia kwenye nyavu za JKT mara 25 huku na wao wakifunga mara 11.

Ramadhan Chombo Redondo Awatahadharisha Young Africans
Ajira: Serikali yatangaza neema ya ajira mpya zaidi ya 71,000 ndani ya mwaka