Kocha Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Dennis Kitambi, amesema kuwa maelekezo waliyowapa wachezaji wao ya kuongeza hali ya kupambana mchezoni kabla ya kuanza kipindi cha pili ndio yamepelekea kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 jana jioni dhidi ya Majimaji ya Songea.

Kitambi amesema pia mabadiliko waliyofanya ya kumwingiza mshambuliaji Ame Ally kipindi cha pili na kumpumzisha Didier Kavumbagu, nayo yamechangia kuondoka na pointi tatu zote katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

“Kwanza nianze kwa kuwapongeza Majimaji kwani walifanikiwa kutukaba kuanzia juu kipindi cha kwanza, walicheza vizuri na awali tulijua kabisa kuwa watakuja na hali ya juu ya kupambana katika mchezo huu, kwa upande wetu sisi kipindi cha kwanza kujituma kwetu hakukuridhisha kwa hiyo hilo lilitufanya tusiweze kufanya vizuri, mapumziko tukaongelea hilo na tukafanya mabadiliko.

“Wachezaji tuliwapa maelekezo ya kuwa tunahitaji hali ya kupambana zaidi kwa sababu kipindi cha kwanza wachezaji wa Majimaji walipambana kupita sisi, kwa hiyo tulivyorudi kipindi cha pili tukapata mabao hayo kupitia kwa Mudathir (Yahya) na tulijua kabisa Majimaji wakirudi kipindi cha pili watashindwa kucheza kwa hali ile ile kwani watakuwa wamechoka,” alisema Kitambi mara baada ya mchezo huo.

NATAKA KUWA KAMA TV YA NYUMBANI KWETU
MTANDAO WA WIZARA KENYA WAVAMIWA