Uchunguzi wa miili ya watu iliyopatikana katika shamba la Mchungaji Paul Mackenzie nchini Kenya, umeonesha baadhi ya waathiriwa walinyongwa na wengine kupigwa.
Wataalam hao, walifanya uchunguzi wa maiti 30, huku Mpasuaji Mkuu wa Serikali, Johansen Oduor, akisema mbali na njaa ilionekana kuwa chanzo kikuu cha vifo kwa baadhi ya waathiriwa ni kuuawa.
Mchungaji Paul Mackenzie. Picha ya Reuters.
Amesema, kati ya miili 40 wanne wakiwemo watoto wawili walionyesha dalili za kukosa hewa, mtoto wa tatu alionekana kupigwa kichwani na kitu butu, huku mtoto wa nne alikabwa hadi kufa.
“Tuliona wazi alama za mtu ambaye amenyongwa na kuvunjika kwa baadhi ya mifupa shingoni, tuna uhakika mtoto huyo alinyongwa,” ameongeza Oduor.
Mchungaji, Ezekiel Odero akiwa chini ya ulinzi. Picha ya Reuters.
Mackenzie anatarajiwa kufikishwa mahakamani ijumaa hii Mei 5, 2023 mjini Mombasa, huku Polisi wakiomba siku 90 za kufanya uchunguzi zaidi kuhusu mauaji hayo ya Shakahola.
Mbali na Mackenzie, Mhubiri mwingine, Ezekiel Odero anakabiliwa na madai yanayomhusisha na kesi ya Mackenzie naye pia atafikishwa mahakamani huku waendesha mashtaka wakisema wana taarifa za maiti zilizofukuliwa Shakahola na vifo vya wafuasi wa Odero.
Sehemu ya miili 109 ambayo ilifukuliwa shambani kwa Mchungaji Paul Mackenzie. Picha ya DN.
Odero ambaye ni mchungaji wa kanisa la New Life Prayer Centre and Church, anashukiwa kwa mauaji, utekaji nyara, itikadi kali, uhalifu dhidi ya binadamu, ukatili wa watoto, ulaghai na utakatishaji fedha.