Tanzani ni nchi yenye vyanzo vingi vya mapato na maliasili ambazo ukizipigia hesabu utagundua kuwa nchi yetu ni tajiri yenye ukwasi wa kutupwa.

Tanzania inamiliki madini ya Tanzanite ambayo hayapo katika nchi yoyote duniani na ni biashara kubwa ya dunia. Kuna migodi ya Nyamamongo, Geita, Mwadui, Buhemba na mingine. Nchi yetu ina mbuga za wanyama, mlima mrefu zaidi Afrika (Kilimanjaro), Maziwa na Bandari kubwa na hivi karibuni tumegundua gesi na madini ya Uranium ambayo ni ‘dili’ kubwa duniani.

Hivyo ni vyanzo vichache sana vya mapato ya nchi yetu ukiweka mbali kodi kutoka kwa makampuni, wafanyabiashara na kodi kutoka kwa wananchi wake. Hapo lazima utakataa ‘katukatu’ ukimsikia mtu anakwambia kuwa ‘Hatuna ubavu wa kujitegemea bila kuomba misaada kutoka nje’.

Rais John Magufuli hivi karibuni amesikika mara kadhaa akisema kuwa Tanzania inapaswa kuwa nchi inayotoa misaada kwa nchi nyingine (donor country) na sio kupigia magoti misaada tunayoipata.

Hata hivyo, pamoja na mambo yote hayo, ukweli ni kwamba Tanzania haiwezi hata kidogo kwa sasa kuwa katika hali iliyopo kiuchumi endapo wahisani na wafadhili wataamua kukata misaada yao na kutuacha tuanze kujitegemea. Tanzania haiwezi kusimama ‘dede’ bila misaada ya wahisani, kwa ufupi hali yetu itakuwa mbaya na mipango na ahadi tulizoahidiwa zinaweza kuota mbawa kwa kipindi cha miaka mitano yote ijayo.

Naona ugumu kwa aya mbili zilizotangulia kupigana vikumbo, yaani ‘sisi sisi ni tajiri’ na ‘hatuwezi kujitegemea’! Huo ndio ukweli unaouma, na hapo ndipo utajiuliza swali kama Mtume Paulo alivyowauliza Wagalatia, “Ni nani aliyewaroga?”

Baada ya Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la Serikali ya Marekani kutangaza kukata mirija ya msaada wake wa zaidi ya shilingi Trilioni 1.3 za Kitanzania zilizokuwa zimeelekezwa kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya umeme vijijini na upanuzi wa barabara, tumesikia kauli mbalimbali za viongozi wetu wakidai hawajashtushwa na haiwaathiri. Hizi kauli nazifananisha na ‘kauli za mkosaji’ au ‘sizitaki mbichi hizi’.

Fikiria mikataba ya miaka 99 tuliyofunga na wawekezaji kwa kutereza. Hii miaka 99 itaisha lini ili tuanze kupata haki yetu tuliyoipoteza kwa makusudi na tuanze kuwabana ili tupate kiburi cha kujitegema? Mikataba mibovu ya migodi itaendelea kututafuna na kibaya zaidi imegeuzwa kuwa ‘siri kubwa’. Hivyo, tunaendelea kutaja maliasili tulizonazo bila kukumbuka kuwa sehemu ya maliasili hiyo iko mikononi mwa ‘mabeberu’ tuliowapa kwa maandishi yetu wenyewe yanayotufunga kitanzi.

Na bahati mbaya hatuwezi kuivunja mikataba hiyo kwa jeuri kuwa tumebaini inatunyonya kwa sababu tuliingia kisheria tukiwa wenye akili timamu!

Tanzania bado haijajiweka katika misingi mikuu ya kuweza kujitegemea na kusimama ‘dede’ ndani ya kipindi cha muda mfupi kuanzia Jumatatu tuliyotangaziwa MCC kukata mrija wake.

Hii ni kwa sababu sio tu kwamba kiasi hicho cha fedha kitaitikisa miradi iliyokusudiwa, bali pia ni alama ya hatari kwa Taifa letu kuanza kupoteza uhalali na sifa za kupokea misaada kutoka kwa mataifa yenye miramba minne kiuchumi (economic giant countries) kama Marekani na washirika wake ambao wana nguvu kubwa.

Kwa bahati mbaya, imejengeka dhana hivi sasa kama vile Marekani iliomba kutupatia fedha za msaada hivyo kama wanaondoka basi imekula kwao. Kumbe sisi wenyewe ndio tuliandika ‘mapropozo’ kuomba msaada husika baada ya kuelezwa fursa hiyo.

Hivyo, kuondoka kwa msaada husika ni kofi la mgeni kwenye uso wa mtu mzima. Sio rahisi kukiri ameumia mbele ya watoto wake.

Tusifikirie kwa fikra za kujipa moyo zaidi, tuangalie pia upande wa pili wa barabara kabla ya kuvuka. Dhana ya kujitegemea isipandikizwe kwa watanzania kama kiini macho cha siasa.

*Kujitegemea sio kubadili wahisani.

Hivi karibuni Mkurugenzi mtendaji wa Tanesco alisema kuwa baada ya MCC kukata mrija wa msaada wake, tayari Tanzania imeshapata njia mbadala ya kiasi hicho cha fedha kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleao ya Afrika (AfDB) kwa ajli ya kusaidia miradi ya umeme vijijini (REA). Je, ndio tumeanza kujitegemea kwa kubadili wahisani?

Hivi kujitegemea ni kumuacha Mmarekani na kuhamia kwa Mchina atupe fedha hizo? Usichoke kujiuliza. Wote tunapenda kujitegemea lakini sio kwa propaganda. Tujenge misingi imara kabla hatujatoka hadharani na kutangaza kujitegemea. Tusitiane moyo kwa nukuu nzuri za viongozi wetu waliopita tunaowaheshimu sana wakati hali halisi inatofautiana na nukuu hizo zenye nia nzuri.

Tunatakiwa kufahamu kuwa, mbali na michango ya misaada kwenye bajeti kuu ya serikali, miradi karibu yote unayoisikia ina pesa za wahisani (Usaid, PFMRP, AfDB, BTC n.k). Nina maanisha ukisikia ‘Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Mkurabita, Mkukuta, Miradi ya Ukimwi, Afya kuhusu magonjwa mbalimbali karibu yote inayoenda moja kwa moja kwa wananchi ni misaada na uhisani wa mataifa yenye miraba minne kiuchumi.

Madaraja makubwa na miradi mingi mikubwa ya ujenzi utasikia nyuma kuna mfadhili na tunaona viongozi wetu wanatiliana sahihi makubaliano na kupiga picha. Tukishangilia tukumbuke kuwa ‘hayo ni mambo ya wahisani/misaada’. Tunatakiwa kujipanga vizuri kabla ya kutangaza tunajitegemea kumbe tunabadili wahisani.

Tunatakiwa kujipanga kwelikweli kwa sababu mipango sio matumizi.

Wapo wanaozungumzia masharti ya msaada wa MCC bila hata kutafuta kujua masharti gani hasa yalitolewa. Msaada wa huo ulikuwa na masharti ambayo yanalinda utu, demokrasia na utawala bora. Hivyo, kujidai haya ni mashati magumu ya wahisani ni kuhalalisha matendo yanayoenda kinyume na hayo.

Tujenge misingi ya kujitegemea kabla hatujaanza vigelegele na propaganda za ‘sizitaki mbichi hizi’.

 

Kiongozi wa Al Shabaab auawa Somalia
Diamond aingia studio na Fally Ipupa, achill na Awilo Longomba