Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ amesema kuwa bajeti ya klabu hiyo katika msimu wa 2019/20 itakuwa mara mbili na nusu ya msimu uliopita.
Ameyasema hayo wakati wa mahojiano na Shirika la Utangazaji la nchini Uingereza BBC, ambapo Dewji amesema kuwa ameyaona mabadiliko makubwa ndani ya kipindi cha msimu mmoja, kitu ambacho kinamfanya azidi kuwa na nguvu ya kuwekeza zaidi ili kufikia kuwa klabu kubwa Afrika.
“Miaka mitano iliyopita, watu walipoteza kabisa matumaini ya kufuatilia klabu na wengi wao walikimbilia kuangali Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, hakuna ambaye alikuwa na habari na Simba, Ndio maana mwaka uliopita tuliweka nguvu kubwa zaidi, tukawaleta wachezaji wakubwa wa Kimataifa, tukatengeneza mfumo wa kusaka wachezaji ‘Scouting’ pamoja na kumpata kocha mkubwa. Bajeti yetu ya msimu uliopita hadi msimu huu imeongezeka mara mbili na nusu,”amesema Dewji.
Aidha, Dewji amesema kuwa alitumia fursa ya kukuza kurasa za mitandao ya kijamii za klabu ya Simba kuwa za kiweledi zaidi pamoja na kuzirasimisha baada ya kuona kwamba Watanzania wengi wanafuatili mitandao ya kijamii, ambapo amesema hatua hiyo imeifanya klabu kukua mara dufu ndani na nje ya nchi.