Balozi Juma Mwapachu, leo amerejea kwenye Chama Cha Mapinduzi baada ya kutangaza kukikacha chama hicho Oktoba 13 mwaka jana, siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Balozi Mwapachu amekabidhiwa tena kadi katika ofisi ya chama hicho iliyoko Mikocheni jijini Dar es Salaam huku akionesha kujuta kukikacha kwa ahadi ya Uwaziri wa Mambo ya Nje aliyopewa na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.

“Baada ya miezi miwili ya uongozi wa Magufuli nataka niseme nilikosea sana. Nililewa mahaba ya Lowasa, nililewa ahadi ya Lowasa kunipa uwaziri wa mambo ya Nje. Niliamini mafuriko ya Lowasa ambayo yakanifanya niamini kabisa anachukua nchi,” alisema Balozi Mwapachu.

Kadhalika, aliweka wazi mpango waliousuka na baadhi ya wanachama wa chama hicho kuondoka kwa mkupuo ili kukitikisa dakika za mwisho na kukifanya kishindwe uchaguzi.

“Tulikubaliana na wenzangu kwamba wiki mbili za mwisho tuihame CCM kwa wimbi kubwa ili kuitikisa na kuitoa madarakani. Lakini baadhi wakaogopa na hadi sasa wengine wamebaki CCM na wana vyeo,” alisema.

Akieleza sababu kuu iliyomvuta kurudi CCM, Balozi Mwapachu alisema kuwa kazi nzuri anayoifanya Rais John Magufuli imemfanya ajute kujiondoa kwa sababu ya mtu, hivyo hanabudi kurudi kwa sababu ya mtu.

“Leo natangaza kurudi CCM kwasababu nimeona kazi nzuri ya Magufuli. Nimefanya kosa kubwa katika siasa ambalo nawasihi vijana kwenye siasa wasifanye. Nilihama kwa kwa sababu ya mtu (Lowassa). Nimerudi kwasababu ya mtu (Magufuli),” anakaririwa.

Mwapachu ambaye anarudi wakati kukiwa na maandalizi ya oparesheni kubwa ya kuwang’oa watu walioisaliti CCM na kumsapoti Lowassa katika uchaguzi mkuu uliopita, amewataka wananchama wa chama hicho kumpokea kwa mikono miwili na kuganga yajayo kwani yaliyopita sio ndwele (sio maradhi ya kuua).

Hata hivyo, amesema kuwa ataendelea kuwa rafiki wa Lowassa kama ilivyokuwa awali japo amerejea kwenye chama chake cha zamani.

 

Ripoti: Tanzania yawa kati ya nchi 10 za mwisho kwa furaha duniani, fahamu sababu
Pluijm Ashanga Al-Ahly Inavyopewa Nafasi Ya Kupambana Na Yanga