Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya (MCK), limeazimia kurudisha kadi zote za idhini ya vyombo vya Habari, ili kuwakabiri wanahabari feki.
Katika taarifa iliyotolewa na Baraza hilo imeeleza kuwa itatoa kadi mpya za vyombo vya habari zenye vipengele vya ziada, ambavyo vitarahisisha kuidhinisha kadi hiyo kwa kutumia simu mahiri yoyote.
“Kadi Mpya za Wanahabari ziwe na vipengele vya ziada ikiwa ni pamoja na msimbo pau na msimbo wa QR unaoweza kuchanganuliwa kwa kutumia simu mahiri yoyote,” ilisema MCK.
Uidhinishaji huo, utasaidia wanahabari kupata habari kwa kuruhusu ushiriki katika makongamano, warsha, mafunzo na mikusanyiko mingine na pia huongeza ulinzi wa haki na marupurupu ya wanahabari katika kutekeleza majukumu yao.
Kulingana na MCK, kada ya watu inastahiki kuidhinisha Waandishi wa habari wanaofanya kazi katika makampuni ya vyombo vya habari, Waandishi wa habari wa kujitegemea, Waandishi wa habari wa kigeni, Wanafunzi wanaofuata masomo ya vyombo vya habari, uandishi wa habari na mawasiliano, Watendaji wa Mahusiano ya Umma, Makampuni ya Utangazaji na Wakufunzi wa Vyombo vya Habari.
Wanahabari watakaoidhinishwa na MCK, wanatakiwa kutoa barua kutoka kwa mwajiri, shahada halisi au cheti cha diploma katika mawasiliano kutoka kwa taasisi inayotambulika.