Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar (SMZ) ambao pia ni wajumbe wa kamati ya Kusimamia viongozi wakuu wa kitaifa wamekutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Masuala ya Muungano na Mazingira January Makamba, Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuzungumzia baadhi ya changamoto za Muungano na kubadilishana mawazo katika maeneo ya Muungano.

Waziri Makamba amewapongeza wajumbe wa Kamati hiyo, na  kusema kuwa ujio wao unaonyesha dhamira nzuri ya kuwawakilisha wananchi wa Zanzibar na kuimarisha Muungano uliodumu kwa muda mrefu kwa sasa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Omary Seif Abeid, ambaye pia ni Muwakilishi wa Jimbo la Konde Pemba, amesema kuwa, pande hizi mbili za Muungano hazina Budi kuwakumbuka waasisi wa Muungano huo Hayati Mzee Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuunganisha pande mbili hizi na kupatikana kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema  kuwa anaebeza Muungano anajibeza mwenyewe.

Hata hivyo kwa pande zote mbili za wajumbe hao wamejadili mambo mbalimbali yanayohusu muungano na kuahidi kudumisha na kufanyia kazi baadhi ya changamoto zinazojitokeza.

Tunajiandaa Kwa ‘Dabi’ Ya Mbeya
NEC yatoa ufafanuzi uchaguzi wa Dimani